Kumbukumbu 4:25-31
Kumbukumbu 4:25-31 NENO
Baada ya kuwa na watoto na wajukuu na kuishi katika nchi hiyo siku nyingi, tena mkijichafua na kutengeneza sanamu ya aina yoyote, mkifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumfanya awe na hasira, ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yenu siku hii kwamba mtaangamia mara moja kutoka katika nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki. Hamtaishi kule kwa muda mrefu bali kwa hakika mtaangamizwa. Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa, na ni wachache wenu tu watakaosalia miongoni mwa mataifa hayo ambayo Mwenyezi Mungu atawafukuzia. Huko mtaabudu miungu ya miti na mawe iliyotengenezwa na watu, ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kula au kunusa. Lakini kama mtamtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mtampata; kama mtamtafuta kwa moyo wote na kwa roho yote. Mnapokuwa katika dhiki, nayo mambo haya yote yamewatokea siku hizo, ndipo mtamrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kumtii. Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ni Mungu mwenye huruma, hatawaacha au kuwaangamiza wala kusahau agano alilofanya na baba zenu, alilowathibitishia kwa kiapo.