Kumbukumbu la Sheria 33:23-29
Kumbukumbu la Sheria 33:23-29 BHN
Juu ya kabila la Naftali alisema: “Ee Naftali fadhili, uliyejaa baraka za Mwenyezi-Mungu, nchi yako ni kusini kwenye ziwa Kinerethi.” Juu ya kabila la Asheri alisema: “Asheri abarikiwe kuliko watoto wote wa Yakobo, na upendelewe na ndugu zako wote; na achovye mguu wake katika mafuta. Miji yako ni ngome za chuma na shaba. Usalama wako utadumu maisha yako yote!” Mose akamalizia kwa kusema, “Ee Israeli, hakuna aliye kama Mungu wako, yeye hupita mbinguni kuja kukusaidia, hupita juu angani katika utukufu wake. Mungu wa milele ndiye kimbilio lenu; nguvu yake yaonekana duniani. Aliwafukuza maadui mbele yenu; aliwaamuru: ‘Waangamizeni.’ Kwa hiyo, watu wa Israeli wakakaa salama, wazawa wa Yakobo peke yao, katika nchi iliyojaa nafaka na divai, nchi ambayo anga lake hudondosha umande. Heri yenu nyinyi Waisraeli. Nani aliye kama nyinyi, watu mliookolewa na Mwenyezi-Mungu, ambaye ndiye ngao ya msaada wenu, na upanga unaowaletea ushindi! Adui zenu watakuja wananyenyekea mbele yenu, nanyi mtawakanyaga chini.”