Kumbukumbu la Sheria 33:1-17
Kumbukumbu la Sheria 33:1-17 BHN
Hii ndiyo baraka ambayo Mose, mtu wa Mungu aliwatakia Waisraeli kabla ya kufariki kwake. Alisema: Mwenyezi-Mungu alikuja kutoka mlima Sinai, alitutokea kutoka mlima Seiri; aliiangaza kutoka mlima Parani. Alitokea kati ya maelfu ya malaika, na moto uwakao katika mkono wake wa kulia. Mwenyezi-Mungu aliwapenda watu wake; na huwalinda watakatifu wake wote. Hivyo, malaika wake walifuata nyayo zake, na kupata maagizo kutoka kwake. Mose alituamuru tutii sheria; kitu cha thamani kuu cha taifa letu. Mwenyezi-Mungu akawa mfalme wa Israeli, wakati viongozi wao walipokutana, na makabila yote yalipokusanyika. Mose alisema juu ya kabila la Reubeni: “Reubeni aishi wala asife, na watu wake wasiwe wachache.” Juu ya kabila la Yuda alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu usikilize kilio cha kabila la Yuda; umrudishe tena kwa watu wale wengine. Upigane kwa mikono yako kwa ajili yake, ulisaidie kabila la Yuda dhidi ya adui zake.” Juu ya kabila la Lawi, alisema: “Ee Mwenyezi-Mungu ulipatie Lawi kauli yako ya Urimu, kauli yako ya thumimu kwa hao waaminifu wako, ambao uliwajaribu huko Masa. Ulishindana nao kwenye maji ya Meriba. Walawi walioamua kuwaacha wazee wao, wakawasahau jamaa zao, wasiwatambue hata watoto wao maana walizingatia amri zako, na kushika agano lako. Na wawafundishe wazawa wa Yakobo maagizo yako; wawafundishe watu wa Israeli sheria yako. Walawi na wafukize ubani mbele yako, sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni pako. Ee Mwenyezi-Mungu, uzibariki nguvu zao, uzikubali kazi za mikono yao; uzivunjilie mbali nguvu za maadui zao, nguvu za wanaowachukia hata wasiinuke tena.” Juu ya kabila la Benyamini alisema: “Hili ni kabila alipendalo Mwenyezi-Mungu, nalo hukaa salama karibu naye. Yeye hulilinda mchana kutwa, na kukaa kati ya milima yake.” Juu ya kabila la Yosefu alisema: “Mwenyezi-Mungu na aibariki nchi yake, kwa baraka nzuri kabisa kutoka juu, ibarikiwe kwa matunda bora yalioiva kwa jua, kwa matunda ya kila mwezi; kwa mazao bora ya milima ya kale, na mazao tele ya milima ya kale, Nchi yake ijae yote yaliyo mema, ibarikiwe kwa wema wa Mwenyezi-Mungu, ambaye alitokea katika kichaka. Baraka hizi ziwashukie watu wa kabila la Yosefu, aliyekuwa mkuu miongoni mwa ndugu zake. Fahari yake ni fahari ya fahali wa kwanza, pembe zake ni za nyati dume. Atazitumia kuyasukuma mataifa; yote atayasukuma mpaka miisho ya dunia. Efraimu atakuwa na pembe hizo 10,000 na Manase kwa maelfu.”