Wakolosai UTANGULIZI
UTANGULIZI
Habari tulizo nazo kuhusu mji wa Kolosai na mahali ulipokuwa ni chache. Lakini inajulikana kwamba ulikuwa yapata kilomita 175 Magharibi ya mji wa Efeso katika mkoa wa Kiroma wa Asia. Wakati mmoja ulikuwa kitovu cha uchumi lakini kuanzia mwaka 61 B.K., baada ya tetemeko kubwa la nchi, ulianza kufifia na hata karibu kutoweka kabisa. Paulo mara kadhaa alipitia sehemu hizo akienda eneo la Frugia (Mate 16:6; 18:23) lakini inaonekana kwamba hakuingia katika mji huo.
Mahubiri ya Habari Njema katika eneo hilo yalifanywa na Epafra ambaye alikuwa mkazi wa Kolosai (4:12) na anachukuliwa kuwa mwanzilishi wa kanisa la Kolosai. Mtume Paulo anamtaja kwa maneno mazuri kama “mtumishi mwenzangu mpenzi” (1:7, rejea File 23) na anamhusisha na jumuiya nyingine mbili za Kikristo: Laodikea na Hierapoli (2:1; 4:13,15-16; rejea Ufu 1:11; 3:14-22). Waumini wa Kolosai hawakuwa Wayahudi.
Ingawa Paulo hakupata kuwatembelea Wakristo wa Kolosai aliwatuma wahudumu wenzake, mmoja wao akiwa Epafra, mwenyeji wa Kolosai. Tukiko anatajwa kwamba ndiye aliyeipeleka barua hii. Paulo, akiwa kifungoni, aliletewa habari na Epafra kwamba Wakristo wa Kolosai walikuwa wanapotoshwa na mafundisho mengine ambayo baadhi yake yalieleza kwamba mtu akitaka kumjua Mungu na kuokolewa sharti aabudu nguvu fulani za kiroho na kutii sheria fulani kama vile kutahiriwa na kutokula vyakula fulanifulani. Basi, Paulo akawaandikia kuwakumbusha kwamba wokovu waliojaliwa na Mungu kwa kuungana na Yesu Kristo ni muhimu na wanapaswa kuzingatia mafundisho ya Yesu peke yake ambaye ndiye mkuu juu ya nguvu zote za kiroho, naye ni kiongozi au kichwa cha Kanisa.
Barua hii yajulikana sana kwa utenzi wake mfupi lakini maalumu kabisa juu ya maumbile yake Yesu Kristo na kazi yake (1:15-20).
Lengo la barua hii ni dhahiri kutokana na yaliyomo. Watu wengine walikuwa wanawafundisha Wakolosai mafundisho yaliyopingana na ujumbe wa Habari Njema ya Kristo. Mafundisho hayo ya uongo yaliyoitwa “falsafa” (2:8) yalihusika na kuamini kwamba kuna roho za ulimwengu ambazo ni lazima ziheshimiwe (2:8,20; Taz pia 1:16; 2:10,15). Vile vile sheria fulani kuhusu vyakula (2:16, 20-21) na sikukuu fulani fulani (2:16b) ni lazima ziheshimiwe.
Sehemu kubwa ya kati ya barua hii (1:9–4:6) yaweza kugawanywa katika sehemu tatu, ikitanguliwa na utangulizi au maneno ya kuanzia (1:1-8) na kumalizia na mawazo ya binafsi na salamu (4:7-18).
Katika sehemu ya kwanza (1:9-23), Paulo anamshukuru Mungu kwa imani na uaminifu wa ndugu walioko kule Kolosai. Sehemu ya pili (1:24–2:5) Paulo anazungumzia juu ya huduma yake ya kitume na mahubiri yake ya Injili kwa watu wa mataifa mengine ambao anawajulisha juu ya mpango wa Mungu uliodhihirishwa katika Kristo aliye tumaini la wote wenye kumwamini. Sehemu ya tatu (2:6–4:6) Paulo anafundisha juu ya umuhimu wa Injili ya neema. Katika Kristo mna ukamilifu wote wa Mungu (2:9).
Iliyochaguliwa sasa
Wakolosai UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.