Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 7

7
MAONO YA HUKUMU
Maono ya kwanza: Nzige
1Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena. 2Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema:
“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie!
Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?
Wao ni wadogo mno!”
3Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,
akasema, “Haitakuwa hivyo!”
Maono ya pili: Moto
4Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu. 5Ndipo nikasema:
“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu!
Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?
Wao ni wadogo mno!”
6Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,
akasema: “Hili pia halitatukia.”
Maono ya tatu: Timazi
7Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi. 8Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema:
“Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli.
Sitavumilia tena maovu yao.
9Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia,
kutafanywa kuwa uharibifu mtupu
na maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu.
Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.”
Amosi na Amazia
10Basi, Amazia kuhani wa mji wa Betheli, akampelekea mfalme Yeroboamu wa Israeli habari hizi: “Amosi analeta fitina juu yako katika ufalme wa Israeli. Hotuba zake ni hatari kwa nchi hii. 11Anachosema ni hiki:
‘Yeroboamu atakufa kwa upanga
nao Waisraeli watapelekwa uhamishoni,
mbali kabisa na nchi yao.’”
12Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Sasa tumekuchoka, ewe nabii! Nenda zako! Rudi katika nchi ya Yuda, ukatoe unabii huko upate na ujira wako hukohuko. 13Usitoe tena unabii hapa mjini Betheli, kwa kuwa hapa ni maskani ya ibada ya mfalme; ni hekalu la utawala huu.”
14Amosi akamjibu Amazia, “Mimi si nabii wa kuajiriwa, wala si mmoja wa kikundi cha manabii. Mimi ni mchungaji na mtunza mikuyu. 15Mwenyezi-Mungu alinitoa katika kazi yangu hiyo ya uchungaji, akaniamuru nije kuwaambia unabii watu wake wa Israeli.
16Nawe basi, ewe Amazia,
sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu:
Wewe waniambia nisitoe unabii dhidi ya Israeli,
wala nisihubiri dhidi ya wazawa wa Isaka.
17Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:
‘Mkeo atakuwa malaya mjini,
na wanao wa kiume na kike watauawa vitani.
Ardhi yako itagawanywa na kupewa wengine,
nawe binafsi utafia katika nchi najisi,
nao Waisraeli hakika watapelekwa uhamishoni,
mbali kabisa na nchi yao.’”

Iliyochaguliwa sasa

Amosi 7: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha