Amosi 3:9-15
Amosi 3:9-15 BHN
Tangazeni katika ikulu za Ashdodi, na katika ikulu za nchi ya Misri: “Kusanyikeni kwenye milima inayoizunguka nchi ya Samaria, mkajionee msukosuko mkubwa na dhuluma zinazofanyika humo.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu hawa wameyajaza majumba yao vitu vya wizi na unyang'anyi. Hawajui kabisa kutenda yaliyo sawa! Kwa hiyo, adui ataizingira nchi yao, atapaharibu mahali pao pa kujihami, na kuziteka nyara ikulu zao.” Mwenyezi-Mungu, asema hivi: “Kama vile mchungaji ampokonyavyo simba kinywani miguu miwili tu au kipande cha sikio la kondoo, ndivyo watakavyonusurika watu wachache tu wa Israeli wakaao Samaria, ambao sasa wanalalia vitanda vizuri na matandiko ya hariri.” Bwana Mungu wa majeshi asema hivi: “Sikilizeni, mkawaonye wazawa wa Yakobo: Siku nitakapowaadhibu Waisraeli kwa sababu ya makosa yao, nitayaharibu pia madhabahu ya mji wa Betheli. Nitazikata pembe za kila madhabahu na kuziangusha chini. Nitaziharibu nyumba zote mjini na vijijini; nitazibomoa nyumba zilizopambwa kwa pembe, majumba makubwamakubwa hayatasalia hata moja. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”