Matendo 5:12-21
Matendo 5:12-21 BHN
Mitume walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana pamoja katika ukumbi wa Solomoni. Mtu yeyote mwingine ambaye hakuwa mwaamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo, watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu. Idadi ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi. Hata watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao. Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kandokando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa. Kisha, kuhani mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu. Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu. Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia, “Nendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uhai huu.” Mitume walitii, wakaingia hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu na halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi, halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume.