Matendo 24:10-21
Matendo 24:10-21 BHN
Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi. Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu. Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu hekaluni, wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo. Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu. Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu wa wazee wetu nikiishi kufuatana na njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya sheria na manabii. Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka. Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu. “Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa tambiko. Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia. Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu. Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu, isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: ‘Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!’”