Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Timotheo 2:7-19

2 Timotheo 2:7-19 BHN

Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uelewe kila kitu. Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri, na ambayo kwa sababu yake mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo. Kwa hiyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele. Usemi huu ni wa kweli: “Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana. Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe.” Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli. Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu. Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto. Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika. Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.”