Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samueli 19:24-39

2 Samueli 19:24-39 BHN

Mefiboshethi mjukuu wa Shauli, alikwenda pia kumlaki mfalme Daudi. Tangu siku ile mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka aliporudi salama, Mefiboshethi alikuwa hajapata kuosha miguu yake, kukata ndevu zake na hakujali kufua nguo zake. Basi, ikawa alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, Daudi alimwuliza, “Je, Mefiboshethi, kwa nini hukuandamana pamoja nami?” Mefiboshethi akasema, “Ee bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya. Maana, mimi mtumishi wako, nilimwambia, ‘Nitandikie punda nipate kumpanda kwenda pamoja na mfalme,’ maana mimi mtumishi wako ni kilema. Sasa, amenisingizia kwako, ee bwana wangu mfalme. Lakini wewe, bwana wangu mfalme, uko kama malaika wa Mungu. Fanya lolote unaloona ni jema kwako. Maana, jamaa yote ya babu yangu walikuwa watu ambao wamestahili kuuawa mbele yako, bwana wangu mfalme. Lakini uliniweka mimi mtumishi wako miongoni mwa wale wanaokula mezani pako. Je, nina haki yoyote zaidi hata nikulilie mfalme?” Mfalme akamwambia, “Usiniambie zaidi juu ya mambo yako ya binafsi. Mimi nimekwisha amua kuwa wewe pamoja na Siba mtagawana nchi ya Shauli.” Lakini Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu Siba aichukue nchi yote peke yake. Mimi nimetosheka kwamba wewe bwana wangu mfalme umerudi nyumbani salama.” Barzilai Mgileadi alikuwa amefika kutoka Rogelimu. Alikuwa amekwenda pamoja na mfalme kwenye mto Yordani ili kumsindikiza hadi ngambo ya mto. Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka themanini. Naye Barzilai alikuwa amemtunza mfalme alipokaa huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa tajiri sana. Basi, mfalme Daudi akamwambia Barzilai, “Twende wote huko Yerusalemu nami nitakutunza.” Lakini Barzilai akamwambia mfalme, “Je, nina miaka mingi ya kuishi ndipo niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu? Mimi leo nina umri wa miaka themanini. Je, nina uwezo wa kubainisha yaliyo mazuri na yale yasiyo mazuri? Je, mimi mtumishi wako, naweza kutambua ladha ya kile ninachokula au kunywa? Je, nitaweza kutambua uzuri wa sauti za waimbaji wanaume au wanawake? Kwa nini mimi mtumishi wako niwe mzigo wa ziada kwako, bwana wangu mfalme? Mimi mtumishi wako nitakwenda nawe mwendo mfupi ngambo ya Yordani. Kwa nini, mfalme anilipe zawadi kubwa hivyo? Nakuomba, uniruhusu mimi mtumishi wako, nifie katika mji wangu, karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu. Lakini huyu mtumishi wako Kimhamu, mruhusu aende pamoja nawe bwana wangu mfalme, na mtendee yeye lolote unaloona ni jema.” Mfalme akamwambia, “Kimhamu atakwenda nami, na nitamtendea lolote lililo jema kwako. Na lolote utakalotaka nikutendee, nitakutendea.” Ndipo watu wote wakavuka mtoni Yordani na mfalme naye akavuka. Mfalme akambusu na kumbariki Barzilai, na Barzilai akarudi nyumbani kwake.