Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 15:17-26

2 Wafalme 15:17-26 BHN

Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka kumi. Alimwasi Mwenyezi-Mungu siku zote za utawala wala hakuacha maovu ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Basi, Pulu mfalme wa Ashuru, aliivamia Israeli, naye Menahemu akampa kilo thelathini na nne za fedha ili amsaidie kuimarisha mamlaka yake juu ya nchi ya Israeli. Menahemu alipata fedha hiyo kwa kuwalazimisha matajiri wa Israeli kutoa mchango wa shekeli hamsini za fedha kila mmoja. Halafu Pulu hakukaa Israeli bali alirudi katika nchi yake. Matendo mengine yote ya Menahemu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli. Menahemu alifariki, naye mwanawe Pekahia alitawala mahali pake. Katika mwaka wa hamsini wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka miwili. Alimwasi Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Peka mwana wa Remalia, ambaye alikuwa ofisa wa jeshi la Pekahia, alishirikiana na watu wengine hamsini kutoka Gileadi, akamuua Pekahia katika ngome ya ndani ya nyumba ya mfalme huko Samaria, na kuwa mfalme mahali pake. Matendo mengine ya Pekahia na yote aliyofanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.