Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 8:1-13

2 Wakorintho 8:1-13 BHN

Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia. Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana. Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe, walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu. Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu. Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia mwitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu. Nyinyi mna kila kitu: Imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo. Siwapi nyinyi amri, lakini nataka tu kuonesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli. Maana, nyinyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: Yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe. Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: Inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Nyinyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo. Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha. Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa; hadai zaidi. Nyinyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wakorintho 8:1-13