2 Mambo ya Nyakati 35:1-19
2 Mambo ya Nyakati 35:1-19 BHN
Mfalme Yosia aliadhimisha Pasaka mjini Yerusalemu, wakachinja wanakondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Aliwateua makuhani kwa kazi zao ambazo walihitajika kufanya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuwatia moyo wazifanye kikamilifu. Pamoja na hayo, aliwapa Walawi waliowafundisha watu wa Israeli na ambao walikuwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, maagizo yafuatayo: “Liwekeni sanduku takatifu ndani ya nyumba ambayo Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli alijenga; hamhitaji kulibebabeba tena mabegani. Sasa mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na watu wake Waisraeli. Timizeni wajibu wenu kulingana na koo zenu, kufuatana na maagizo ya Daudi mfalme wa Israeli na Solomoni mwanawe. Simameni pia mahali patakatifu kama wawakilishi wa jamaa za koo zenu wasiofanya kazi za ukuhani, na kila mmoja aiwakilishe jamaa moja ya Walawi. Mchinjeni mwanakondoo wa Pasaka, mjitakase, halafu itayarisheni kwa ajili ya ndugu zenu, ili waweze kutimiza agizo la Mwenyezi-Mungu lililosemwa na Mose.” Kisha Yosia aliwapa watu, wanambuzi wapatao 30,000, na mafahali 3,000, wote hawa walitolewa kwenye mifugo ya mfalme. Nao maofisa wake, kwa hiari yao, walitoa mchango wao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, maofisa wa nyumba ya Mungu, waliwapa makuhani wanakondoo na wanambuzi 2,600 na mafahali 300 kwa ajili ya sadaka za Pasaka. Naye Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi, waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia waliwapa wanakondoo na wanambuzi 5,000 na mafahali 500, kwa ajili ya sadaka za Pasaka. Baada ya matayarisho yote ya Pasaka kumalizika, makuhani walisimama mahali pao, na Walawi katika makundi yao; sawasawa na amri ya mfalme. Walimchinja mwanakondoo wa Pasaka, nao makuhani walinyunyiza damu, waliyopokea kutoka kwao nao Walawi waliwachuna wanyama. Halafu walitenga sadaka za kuteketeza ili waweze kuzigawa kulingana na jamaa zao walio makuhani ili wamtolee Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nayo mafahali waliwafanya vivyo hivyo. Walimchoma mwanakondoo wa Pasaka juu ya moto kama ilivyoagizwa, na pia walizitokosa sadaka takatifu katika vyungu, masufuria na kwenye vikaango, na kuwagawia upesiupesi watu wasiofanya kazi ya ukuhani. Baadaye, Walawi wakajiandalia sehemu zao na za makuhani kwa maana makuhani wa uzao wa Aroni walikuwa wanashughulika na utoaji wa sadaka za kuteketeza, na vipande vya mafuta, mpaka usiku; kwa hiyo Walawi waliandaa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni. Nao waimbaji wazawa wa Asafu walishika nafasi zao, kwa mujibu wa maagizo ya mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni, mwonaji wa mfalme. Nao mabawabu walikuwa kwenye malango; hawakuhitajika kuziacha nafasi zao za kazi kwa kuwa ndugu zao Walawi waliwaandalia Pasaka. Hivyo basi, huduma yote ya Mwenyezi-Mungu ilitayarishwa siku hiyo, ili kuiadhimisha Pasaka na kutoa sadaka za kuteketeza kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamuru mfalme Yosia. Wakati huo watu wote wa Israeli waliohudhuria waliiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa muda wa siku saba. Pasaka kama hiyo ilikuwa haijasherehekewa katika Israeli yote tangu siku za nabii Samueli. Hapajatokea mfalme hata mmoja wa Israeli aliyeadhimisha Pasaka kama hii iliyoadhimishwa na mfalme Yosia pamoja na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda, watu wa Israeli na wakazi wa Yerusalemu. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia.