2 Mambo ya Nyakati 32:27-31
2 Mambo ya Nyakati 32:27-31 BHN
Mfalme Hezekia alitajirika sana, akaheshimiwa. Alijitengenezea hazina za fedha, za dhahabu, za vito, za viungo, ngao na za aina zote za vyombo vya thamani kubwa. Aidha, alijijengea mabohari ya kuhifadhia mazao ya nafaka, divai na mafuta, na mazizi kwa ajili ya ng'ombe na mengine kwa ajili ya kondoo. Vivyo hivyo alijiongezea miji kwa ajili yake mwenyewe, makundi mengi ya ng'ombe na kondoo kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimkirimia mali nyingi. Mfalme Hezekia ndiye aliyeyafunga maji ya chemchemi ya Gihoni, akayachimbia mfereji wa chini kwa chini hadi upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Hezekia alifaulu katika kila jambo alilofanya, na hata wakati ambapo mabalozi wa wakuu wa Babuloni waliotumwa kwake kuuliza juu ya mambo ya ajabu yaliyotokea humo, Mungu, alimwacha ajiamulie mwenyewe, ili amjaribu na kujua yote yaliyokuwa moyoni mwake.