1 Timotheo UTANGULIZI
UTANGULIZI
Timotheo alikuwa mwana wa mama mmoja Myahudi na baba yake alikuwa Mgiriki. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume na katika barua nyingine za Paulo, tunajua kwamba Timotheo aliandamana na Paulo katika ziara zake na kumsaidia katika kazi yake ya kuhubiri Habari Njema (taz Mate 17:14-15; 18:5; 19:22 na 1Kor 4:17; 16:10-11; Fil 2:19-24; n.k.). Barua hii ya kwanza na ile ya pili pamoja na barua kwa Tito zaitwa pia barua za “kichungaji” kwa vile zinawapa mwongozo hao “wachungaji” au viongozi wa Kanisa.
Barua hii ya kwanza kwa Timotheo yahusu mambo matatu makubwa:
Kwanza Paulo anaonya jumuiya ya Wakristo ijihadhari na mafundisho ya uongo yaliyochanganya fikira za Kiyahudi na za watu wasio Wayahudi, mafundisho ambayo yalikuwa yanaendelezwa na baadhi ya watu. Baadhi ya mafundisho hayo yaliwaaminisha watu kwamba ulimwengu huu unaoonekana ni mbaya na kwamba mtu anaweza tu kuokoka kwa kujua siri fulani ambazo wamepewa tu watu fulani. Zaidi ya hayo watu walitakiwa kufuata mazoezi yaliyohusika na kuacha kula vyakula fulanifulani. Kisha Paulo anatoa mwongozo kuhusu ibada, muundo na mpango katika jumuiya ya Wakristo au Kanisa na tabia ya viongozi wake.
Mwisho anatoa mashauri yake kwa Timotheo kuhusu namna ya kutekeleza utumishi wake na kujishughulisha na makundi mbalimbali ya waumini ili apate kuwa kweli “mtumishi mwema wa Kristo Yesu” (4:6).
Iliyochaguliwa sasa
1 Timotheo UTANGULIZI: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.