Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:1-21

1 Wafalme 8:1-21 BHN

Basi, mfalme Solomoni akawakutanisha mbele yake huko Yerusalemu wazee na viongozi wote wa makabila na wa koo za Israeli ili waliondoe sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu katika mji wa Daudi, yaani Siyoni. Wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, yaani mwezi wa saba. Ndipo watu hao wote walipokusanyika mbele ya mfalme Solomoni. Baada ya wazee wote wa Israeli kuwasili, makuhani walibeba sanduku la agano. Walawi na makuhani walihamisha sanduku la agano na hema la mkutano, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa humo hemani. Mfalme Solomoni na mkutano wote wa Israeli wakakusanyika mbele ya sanduku la agano, nao wakatoa tambiko: Ng'ombe na kondoo wasiohesabika. Kisha makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu mahali pake, katika chumba cha ndani cha nyumba mahali patakatifu sana, chini ya mabawa ya viumbe wenye mabawa. Hao viumbe wenye mabawa walitandaza mabawa yao juu ya mahali lilipowekwa sanduku, kwa hiyo sanduku na mipiko yake ya kulibebea vilikuwa chini ya mabawa. Kwa kuwa mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana, ncha zake ziliweza kuonekana kutoka mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini haikuweza kuonekana kutoka upande wa nje. Mipiko hiyo ingali mahali hapo hata leo. Hapakuwa na kitu ndani ya sanduku la agano ila vile vibao viwili vya mawe ambavyo Mose aliviweka humo kule Horebu, mahali Mwenyezi-Mungu alipofanya agano na Waisraeli walipotoka nchini Misri. Ikawa, makuhani walipotoka pale mahali patakatifu, wingu liliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani walishindwa kuhudumu kwa sababu ya wingu hilo; kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Ndipo Solomoni akasema, “Mwenyezi-Mungu alisema kwamba, atakaa katika giza nene. Hakika, nimekujengea nyumba ya kukaa, mahali pa makao yako ya milele.” Kisha, Solomoni akaigeukia jumuiya yote ya Waisraeli wakiwa wamesimama, akawabariki, akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ametimiza ahadi yake aliyompa baba yangu Daudi, akisema: ‘Tangu niwaondoe watu wangu Israeli nchini Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; ila nilimchagua Daudi, atawale watu wangu, Israeli.’ Kwa hiyo, baba yangu alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba. Hata hivyo, si wewe utakayenijengea nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’ Na sasa, Mwenyezi-Mungu ametimiza ahadi yake, kwani nimekuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, na kukikalia kiti cha enzi cha Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyoahidi; pia nimejenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Zaidi ya hayo, nimetenga mahali pa kuweka sanduku la agano ambalo ndani yake mna agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na babu zetu, wakati alipowatoa katika nchi ya Misri.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 8:1-21