1 Wafalme 21:17-29
1 Wafalme 21:17-29 BHN
Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Elia wa Tishbe: “Inuka uende kukutana na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye yuko Samaria. Utamkuta katika shamba la mizabibu la Nabothi, akilimiliki. Mwambie, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Umeua na kumiliki pia?’ Mwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, ndipo watakapoilamba damu yako.’” Basi, Ahabu alipomwona Elia, akasema, “Ewe adui yangu, umenifuma?” Elia akamjibu, “Naam! Nimekufuma, kwa sababu wewe umenuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Haya! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Hakika, nitakuletea maangamizi. Nitakuzoa wewe na kufutilia mbali kila mwanamume wa ukoo wako katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa yako nitaifanya kama jamaa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama jamaa ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umeiwasha hasira yangu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.’ Tena, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Yezebeli: ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli humuhumu mjini Yezreeli. Naam, yeyote wa jamaa yake atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.’” (Hakuna mtu aliyenuia kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Ahabu, ambaye alishawishiwa na Yezebeli, mkewe. Alitenda machukizo kwa kuabudu sanamu za miungu kama walivyofanya Waamori ambao hapo awali Mwenyezi-Mungu aliwafukuza mbele ya watu wa Israeli). Lakini, Ahabu aliposikia maneno hayo, alirarua nguo zake, akajivalia gunia peke yake, akafunga, akawa analala na gunia, na kwenda huko na huko kwa huzuni. Basi, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Elia wa Tishbe: “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekesha mbele yangu? Basi, kwa kuwa amejinyenyekesha, sitaleta yale maangamizi akiwa hai, lakini nyakati za utawala wa mwanawe nitaiangamiza jamaa yake Ahabu.”