1 Wafalme 21:17-29
1 Wafalme 21:17-29 SRUV
Neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena BWANA alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla. (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.) Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la BWANA likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.