1 Wafalme 20:23-34
1 Wafalme 20:23-34 BHN
Watumishi wa mfalme Ben-hadadi walimshauri hivi: “Miungu ya Waisraeli ni miungu ya milimani; ndiyo maana tulishindwa. Lakini, bila shaka tutawashinda kama tukipigana nao mahali tambarare. Sasa, wastaafishe wale wafalme thelathini na wawili na mahali pao uweke majemadari. Unda jeshi kama lilelile ulilopoteza, farasi na magari ya kukokotwa kama yale uliyopoteza. Kisha, tutapigana nao mahali tambarare na bila shaka tutawazidi nguvu.” Mfalme Ben-hadadi akasikia ushauri wao, akafanya hivyo. Mara baada ya majira ya baridi, mfalme Ben-hadadi aliwakusanya watu wake, akaenda mjini Afeka kupigana na watu wa Israeli. Nao watu wa Israeli walikusanywa na kupewa silaha, wakaenda kuwakabili Waaramu. Watu wa Israeli walipiga kambi, wakaonekana kama vikundi vidogovidogo vya mbuzi, lakini Waaramu walitapakaa kote nchini. Ndipo, mtu mmoja wa Mungu akamkaribia mfalme wa Israeli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa kuwa Waaramu wamesema kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wa milimani wala si Mungu wa nchi tambarare, nitakupa ushindi dhidi ya jeshi hili kubwa, nawe utatambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.’” Watu wa Israeli na Waaramu walipiga kambi kwa muda wa siku saba, wakikabiliana; siku ya saba, mapigano yakaanza. Siku hiyohiyo, watu wa Israeli wakaua askari wa miguu 100,000. Waliosalia, walikimbilia mjini Afeka. Huko, kuta za mji ziliwaangukia na kuwaua watu 27,000 waliobakia. Ben-hadadi pia alikimbia na kujificha katika chumba fulani cha ndani, mjini. Watumishi wake wakamwendea wakamwambia, “Tumesikia kwamba wafalme wa Israeli ni watu wenye huruma. Basi, turuhusu tujifunge magunia viunoni na kamba shingoni, tumwendee mfalme wa Israeli. Huenda atayasalimisha maisha yako.” Basi, wakajifunga magunia viunoni na kamba shingoni mwao, wakamwendea mfalme wa Israeli, wakamwambia, “Mtumishi wako, Ben-hadadi, anakusihi akisema ‘Tafadhali uniache nipate kuishi.’ Ahabu akasema, ‘Kumbe anaishi bado? Yeye ni ndugu yangu.’” Watumishi wa Ben-hadadi walikuwa wanategea ishara yoyote ile ya bahati njema, basi Ahabu aliposema hivyo, wao wakadakia wakasema, “Naam, Ben-hadadi ni ndugu yako!” Ahabu akawaambia, “Nendeni mkamlete kwangu.” Basi, Ben-hadadi alipomjia, Ahabu akamtaka aketi naye katika gari lake la kukokotwa. Kisha, Ben-hadadi akamwambia, “Miji yote ambayo baba yangu alimnyanganya baba yako, nitakurudishia. Unaweza kuanzisha masoko huko Damasko kama alivyofanya baba yangu huko Samaria.” Ahabu akajibu, “Nitakuachilia kwa masharti hayo.” Hapo, akafanya mkataba naye na kumwacha huru.