Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 19:3-18

1 Wafalme 19:3-18 BHN

Elia akakimbilia mjini Beer-sheba mkoani Yuda, alikomwacha mtumishi wake, naye akatembea mwendo wa siku nzima kuingia jangwani. Basi, akafika, akaketi chini ya mti mmoja, mretemu. Hapo, akaomba afe, akisema, “Imetosha! Siwezi tena. Ee Mwenyezi-Mungu, sasa utoe uhai wangu. Mimi si bora kuliko wazee wangu.” Basi, Elia akalala chini ya mti huo, akashikwa na usingizi. Punde, malaika akaja, akamgusa na kumwambia, “Amka ule.” Elia alipotazama, akaona mkate uliookwa juu ya makaa, na chupa ya maji karibu na kichwa chake. Basi, akala, akanywa, akalala tena. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamjia tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Amka ule, la sivyo safari itakuwa ngumu mno kwako.” Elia akaamka, akala na kunywa. Kisha akatembea kwa nguvu ya chakula hicho mwendo wa siku arubaini, mchana na usiku, mpaka Horebu, mlima wa Mungu. Huko, akafika penye pango, akakaa humo. Mara neno la Mwenyezi-Mungu likamjia: “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ewe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda ukasimame mlimani, mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akapita na kuuvumisha upepo mkali ambao uliporomosha milima na kuvunja miamba. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika upepo huo. Upepo ukapita, kukawa na tetemeko la ardhi. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika tetemeko la ardhi. Tetemeko likapita, kukawa na moto. Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwemo katika moto huo. Baada ya moto, pakatokea sauti ndogo, tulivu. Basi, Elia aliposikia sauti hiyo, alijifunika uso kwa joho lake, akatoka na kusimama mlangoni mwa pango. Hapo, akasikia sauti, “Elia! Unafanya nini hapa?” Naye akasema, “Naona uchungu na wivu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, kwa sababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda waniue!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako. Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua. Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wafalme 19:3-18

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha