1 Wafalme 12:6-15
1 Wafalme 12:6-15 BHN
Baadaye Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake Solomoni, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?” Wazee hao wakamjibu, “Leo ukiwa mtumishi wa watu hawa, ukawatumikia na kuongea nao vizuri unapowajibu, hapo watakuwa watumishi wako daima.” Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee; badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake. Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia niwapunguzie mzigo ambao baba yangu aliwatwika?” Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia baba yako aliwatwika mzigo mzito, wakakuomba uwapunguzie mzigo huo, wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu. Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’” Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza. Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee, akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.” Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo.