Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 14:1-25

1 Wakorintho 14:1-25 BHN

Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu. Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo. Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa. Basi, ningependa nyinyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa. Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani. Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa? La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita? Hali kadhalika na nyinyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani. Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana. Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu. Hali kadhalika na nyinyi, maadamu mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa. Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua. Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure. Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu. Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema: “Amina”, kama haelewi unachosema? Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini huyo mwingine haitamfaidia. Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni kuliko nyinyi nyote. Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema maneno elfu ya lugha ngeni. Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu, muwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu waliokomaa. Imeandikwa katika sheria: “Bwana asema hivi: ‘Kwa njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza.’” Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili ya wasioamini. Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je, hawatasema kwamba nyinyi mna wazimu? Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu. Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na kumwabudu Mungu akisema: “Kweli Mungu yupo pamoja nanyi.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wakorintho 14:1-25