Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 14:1-25

1 Wakorintho 14:1-25 NEN

Fuateni upendo na kutaka sana karama za roho, hasa karama ya unabii. Kwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho. Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili kanisa lipate kujengwa. Sasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho? Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji? Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita? Vivyo hivyo na ninyi, kama mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu. Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana. Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu. Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa. Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena. Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda. Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia. Ikiwa unabariki kwa roho, mtu mwingine atakayejikuta miongoni mwa hao wasiojua, atawezaje kusema “Amen” katika kushukuru kwako, wakati haelewi unachosema? Mnaweza kuwa mnatoa shukrani kweli, sawa, lakini huyo mtu mwingine hajengeki. Namshukuru Mungu kwamba mimi nanena kwa lugha kuliko ninyi nyote. Lakini ndani ya kanisa ni afadhali niseme maneno matano ya kueleweka ili niwafundishe wengine kuliko kusema maneno 10,000 kwa lugha. Ndugu zangu, msiwe kama watoto katika kufikiri kwenu, afadhali kuhusu uovu mwe kama watoto wachanga, lakini katika kufikiri kwenu, mwe watu wazima. Katika Sheria imeandikwa kwamba: “Kupitia kwa watu wenye lugha ngʼeni na kupitia midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, lakini hata hivyo hawatanisikiliza,” asema Bwana. Basi kunena kwa lugha ni ishara, si kwa watu waaminio, bali kwa wasioamini, wakati unabii si kwa ajili ya wasioamini, bali kwa ajili ya waaminio. Kwa hiyo kama kanisa lote likikutana na kila mmoja akanena kwa lugha, kisha wakaingia wageni wasioelewa wasioamini, je, hawatasema kwamba wote mna wazimu? Lakini kama mtu asiyeamini au asiyeelewa akiingia wakati kila mtu anatoa unabii, ataaminishwa na watu wote kuwa yeye ni mwenye dhambi na kuhukumiwa na wote, nazo siri za moyo wake zitawekwa wazi. Kwa hiyo ataanguka chini na kumwabudu Mungu akikiri, “Kweli Mungu yuko katikati yenu!”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Wakorintho 14:1-25