1 Mambo ya Nyakati 29:1-9
1 Mambo ya Nyakati 29:1-9 BHN
Mfalme Daudi akaumbia ule mkutano wote uliojumuika, “Solomoni, mwanangu, ambaye peke yake amechaguliwa na Mungu, bado yungali mdogo, na hana uzoefu mwingi, na kazi hii ni kubwa. Nyumba atakayoijenga si ya mwanadamu, bali ni ya Mungu, Mwenyezi-Mungu. Basi, nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote kuiwekea nyumba ya Mungu wangu, akiba ya dhahabu ya kutengenezea vitu vya dhahabu, fedha ya kutengenezea vitu vya fedha, shaba ya kutengenezea vitu vya shaba, chuma cha kutengenezea vitu vya chuma, na miti ya kutengenezea vitu vya miti. Zaidi ya hayo, nimevitayarisha kwa wingi vito vya rangi na mawe ya kujazia vito vya njumu, mawe ya rangi, mawe ya thamani ya kila namna na marumaru. Tena, zaidi ya vyote nilivyotoa kwa ajili ya nyumba takatifu, ninayo hazina yangu binafsi ya dhahabu na fedha, na kwa sababu naipenda nyumba ya Mungu wangu, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu: Tani 3,000 za dhahabu kutoka Ofiri, talanta 700 za fedha safi ya kuzifunikia kuta za nyumba, na kwa ajili ya kutengenezea vitu vya kila aina vitakavyotengenezwa na mafundi kwa mikono. Nimeweka dhahabu kwa ajili ya vyombo vya dhahabu, na fedha kwa ajili ya vyombo vya fedha. Ni nani basi atakayemtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari ili ajiweke wakfu hivi leo kwa Mwenyezi-Mungu?” Ndipo wakuu wa koo, viongozi wa makabila ya Israeli, makamanda wa maelfu na wa mamia; pia na maofisa wasimamizi wa kazi za mfalme walipotoa kwa hiari yao. Walitoa kwa ajili ya huduma za nyumba ya Mungu: Tani 170 za dhahabu, tani 340 za fedha, tani 620 za shaba na tani 3,400 za chuma. Wale ambao walikuwa na vito vya thamani walivitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo watu wakafurahi kwa sababu walitoa kwa hiari, maana kwa moyo wao wote walimtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari, naye mfalme Daudi alifurahi sana.