1 Mambo ya Nyakati 11:10-25
1 Mambo ya Nyakati 11:10-25 BHN
Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli. Ifuatayo ni orodha ya mashujaa hao wa Daudi: Yashobeamu, Mhakmoni, aliyekuwa kiongozi wa “Wale thelathini.” Yeye alipigana kwa mkuki wake akaua watu 300 kwa mara moja vitani. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, Mwahohi. Siku moja Eleazari alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-damimu, wakati Wafilisti walipokusanyika kupigana vita. Huko kulikuwa na shamba lenye shayiri tele, nao Waisraeli walikuwa wamewakimbia Wafilisti. Lakini Daudi na Eliazari walisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, wakawaua Wafilisti; Mwenyezi-Mungu akawaokoa kwa kuwapa ushindi mkubwa. Kisha mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka hadi kwenye mwamba, wakamwendea Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti kama mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu kilicho karibu na lango la mji!” Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa, na badala yake akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu akisema, “Tendo kama hili lipitishie mbali nami; siwezi kulifanya mbele ya Mungu wangu. Je, waweza kunywa damu ya maisha ya watu hawa? Maana kwa kuyahatarisha maisha yao walileta maji haya.” Kwa hiyo Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndio mambo waliyotenda wale mashujaa watatu. Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa thelathini, hata akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Naye Benaya, mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa barafu, alishuka na kuua simba shimoni. Vilevile, alimuua Mmisri mmoja, mtu mrefu sana, urefu wake kama mita mbili, naye mkononi mwake alikuwa amebeba mkuki mkubwa sana, kama mti wa mfumaji. Lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumuua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi.