Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 11:10-25

1 Nyakati 11:10-25 NENO

Hawa walikuwa wakuu wa mashujaa wa Daudi: wao pamoja na Waisraeli wote wakauimarisha ufalme wake ili kuenea katika nchi yote, sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu aliloahidi. Hii ndio orodha ya mashujaa wa Daudi: Yashobeamu Mhakmoni alikuwa mkuu wa maafisa; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, aliowaua katika pambano moja. Aliyefuata alikuwa Eleazari, mwana wa Dodai Mwahohi, mmoja wa wale mashujaa watatu. Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-Damimu, wakati Wafilisti walikusanyika huko kwa ajili ya vita. Mahali palipokuwa na shamba limejaa shayiri, vikosi vya Israeli vikawakimbia Wafilisti. Lakini Eleazari na Daudi wakasimama imara katikati ya lile shamba, nao wakalishindania na kuwaua Wafilisti. Naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa. Wakuu watatu miongoni mwa wale thelathini walimwendea Daudi kwenye mwamba, katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti walikuwa wamepiga kambi katika Bonde la Warefai. Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilichoko karibu na lango la Bethlehemu!” Kwa hivyo wale watatu, wakapita katikati ya safu za Wafilisti, wakachota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Akasema, “Mungu apishie mbali kwamba nifanye hivi! Je kweli, niinywe damu ya watu hawa waliohatarisha maisha yao?” Kwa sababu walihatarisha maisha yao kuyaleta yale maji, Daudi hakukubali kuyanywa. Huo ndio uliokuwa ujasiri wa wale mashujaa watatu. Abishai, ndugu yake Yoabu ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu, ambao aliwaua; kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. Alitunukiwa heshima maradufu ya wale Watatu, akawa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao. Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. Alimuua Mmisri aliyekuwa na urefu kama dhiraa tano. Ingawa huyo Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi, Benaya alimwendea na rungu. Akamnyang’anya Mmisri mkuki wake na kumuua nao. Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu: Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.