Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 24

24
Isa afufuka
(Mathayo 28:1-10; Marko 16:1-8; Yohana 20:1-10)
1Siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini. 2Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka mdomo wa kaburi, 3lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Isa. 4Walipokuwa wanashangaa kuhusu jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayong’aa kama umeme wakasimama karibu nao. 5Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao hadi chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu? 6Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: 7‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” 8Ndipo wakayakumbuka maneno ya Isa.
9Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. 10Basi Mariamu Magdalene, Yoana, na Mariamu mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi. 11Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi. 12Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.
Isa awatokea wanafunzi wawili
(Marko 16:12-13)
13Ikawa siku hiyo hiyo, wanafunzi wawili wa Isa walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba#24:13 kama kilomita 11 kutoka Yerusalemu. 14Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. 15Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Isa mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, 16lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.
17Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?”
Wakasimama, nyuso zao zikionesha huzuni. 18Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiwe peke yako mgeni huku Yerusalemu, ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?”
19Akawauliza, “Mambo gani?”
Wakamjibu, “Mambo ya Isa Al-Nasiri. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. 20Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. 21Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatendeke. 22Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walienda kaburini leo alfajiri, 23lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Isa yu hai. 24Kisha baadhi ya wenzetu walienda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.”
25Isa akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! 26Je, haikumpasa Al-Masihi#24:26 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta. kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” 27Naye akianzia na Torati ya Musa na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu.
28Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Isa akawa kama anaendelea mbele. 29Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao.
30Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. 31Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. 32Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?”
33Wakaondoka mara hiyo, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao wamekusanyika, 34wakasema, “Ni kweli! Bwana Isa amefufuka, naye amemtokea Simoni.” 35Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Isa alipoumega mkate.
Isa awatokea wanafunzi wake
(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)
36Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Isa mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
37Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. 38Lakini Isa akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu? 39Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi mwenyewe. Niguseni mwone; kwa maana mzuka huna nyama na mifupa, kama mnavyoniona mimi.”
40Aliposema haya, akawaonesha mikono na miguu yake. 41Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?”
42Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, 43naye akakichukua na kukila mbele yao.
44Akawaambia, “Haya ndio yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu katika Torati ya Musa, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”
45Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko Matakatifu. 46Akawaambia, “Haya ndio yaliyoandikwa: Al-Masihi atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49“Tazama nitawatumia ahadi ya Baba#24:49 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo kutoka juu.”
Isa apaa mbinguni
(Marko 16:19-20; Matendo 1:9-11)
50Baada ya kuwaongoza hadi Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki. 51Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni. 52Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 24: ONMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia