Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 31

31
Yakobo akimbia kutoka kwa Labani
1Yakobo akawasikia wana wa Labani wakisema, “Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu, naye amepata utajiri huu wote kutokana na mali ya baba yetu.” 2Yakobo akatambua kwamba moyo wa Labani kwake umebadilika.
3Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.”
4Hivyo Yakobo akatuma ujumbe kwa Raheli na Lea waje malishoni kwenye makundi yake. 5Akawaambia, “Naona moyo wa baba yenu kwangu umebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. 6Mnajua kwamba nimemtumikia baba yenu kwa nguvu zangu zote, 7lakini baba yenu amenidanganya kwa kubadilisha ujira wangu mara kumi. Hata hivyo, Mungu hakumruhusu kunidhuru. 8Aliposema, ‘Wenye madoadoa watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye madoadoa. Aliposema, ‘Wenye mistari watakuwa ujira wako,’ basi makundi yote yalizaa wenye mistari. 9Hivyo Mungu amechukua mifugo ya baba yenu na amenipa mimi.
10“Majira ya kuzaliana niliota ndoto. Niliinua macho na kuona kwamba wale beberu waliokuwa wakiwapanda mbuzi walikuwa wana mistari, madoadoa na mabaka mabaka. 11Malaika wa Mungu akaniita katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’ 12Akaniambia, ‘Inua macho yako uone wale beberu wote wanaowapanda mbuzi wana mistari, madoadoa au mabaka mabaka, kwa maana nimeona yale yote Labani amekutendea. 13Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia nguzo mafuta, na ukaniwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ”
14Ndipo Raheli na Lea wakajibu, “Je bado tunalo fungu lolote katika urithi wa nyumba ya baba yetu? 15Je, yeye hatuhesabu sisi kama wageni? Sio kwamba ametuuza tu, bali ametumia hata mali tuliyolipiwa. 16Hakika utajiri wote ambao Mungu ameuchukua kutoka kwa baba yetu ni mali yetu na watoto wetu. Hivyo fanya lolote lile Mungu alilokuambia.”
17Ndipo Yakobo akawapandisha watoto wake na wake zake juu ya ngamia. 18Naye akawaswaga wanyama wote mbele yake, pamoja na mali yote aliyokuwa amepata huko Padan-Aramu ili aende kwa baba yake Isaka katika nchi ya Kanaani.
19Labani alipokuwa ameenda kukata kondoo wake manyoya, Raheli aliiba miungu ya nyumbani mwa baba yake. 20Zaidi ya hayo, Yakobo alimdanganya Labani Mwaramu#31:20 au Mshami kwa kutokumwambia kwamba anakimbia. 21Hivyo akakimbia pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo na kuvuka Mto#31:21 yaani Mto Frati, akaelekea nchi ya vilima ya Gileadi.
Labani amfuatilia Yakobo
22Siku ya tatu, Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia. 23Akiwachukua jamaa zake, akamfuatia Yakobo kwa siku saba na kumkuta kwenye nchi ya vilima ya Gileadi. 24Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”
25Yakobo alikuwa amepiga hema lake katika nchi ya vilima ya Gileadi wakati Labani alimfikia; naye Labani na jamaa yake wakapiga kambi huko pia. 26Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Umenidanganya na umewachukua binti zangu kama mateka katika vita. 27Kwa nini ulikimbia kwa siri na kunidanganya? Kwa nini hukuniambia ili nikuage kwa furaha na nyimbo za matari na vinubi? 28Hata hukuniruhusu niwabusu wajukuu zangu na kuwaaga binti zangu. Umefanya kitu cha kipumbavu. 29Nina uwezo wa kukudhuru, lakini usiku uliopita Mungu wa baba yako alisema nami, akaniambia, ‘Jihadhari, usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.’ 30Sasa umeondoka kwa sababu umetamani kurudi nyumbani mwa baba yako. Lakini kwa nini umeiiba miungu yangu?”
31Yakobo akamjibu Labani, “Niliogopa, kwa sababu nilifikiri ungeweza kuninyang’anya binti zako kwa nguvu. 32Lakini ukimkuta yeyote na miungu yako, huyo mtu hataishi. Mbele ya jamaa zetu, angalia mwenyewe uone kama kuna chochote chako hapa nilicho nacho; kama kipo, kichukue.” Basi Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiiba hiyo miungu.
33Kwa hiyo Labani akaingia ndani ya hema la Yakobo, na ndani ya hema la Lea, na ndani ya hema la wajakazi wale wawili, lakini hakuipata hiyo miungu. Baadaye alipotoka hema la Lea, akaingia hema la Raheli. 34Basi Raheli ndiye alikuwa ameichukua ile miungu ya nyumbani mwao na kuiweka katika matandiko ya ngamia, na kukalia. Labani akatafuta kila mahali kwenye hema lakini hakupata chochote.
35Raheli akamwambia baba yake, “Usikasirike bwana wangu, kwa kuwa siwezi kusimama ukiwepo, niko katika hedhi.” Labani akatafuta lakini hakuweza kuipata miungu ya nyumbani mwake.
36Yakobo akakasirika na kumshutumu Labani, akisema, “Uhalifu wangu ni nini?” Akamuuliza Labani, “Ni dhambi gani niliyofanya hata unaniwinda? 37Sasa kwa kuwa umepekua vitu vyangu vyote, umepata nini kilicho cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya jamaa yako na yangu, nao waamue kati yetu.
38“Hadi sasa nimekuwa pamoja nawe miaka ishirini. Kondoo wako na mbuzi wako hawajaharibu mimba, wala sijala kondoo dume kutoka makundi yako. 39Sijakuletea mfugo aliyeraruliwa na wanyama pori, bali nimegharimia hasara mwenyewe. Tena umenidai malipo kwa chochote kilichoibwa mchana au usiku. 40Hali yangu imekuwa hivi: Nimechomwa kwa joto la mchana, na kupigwa na baridi usiku, pia usingizi ulinipotea. 41Imekuwa hivi kwa miaka ile ishirini niliyokuwa nyumbani kwako. Nilikutumikia miaka ile kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya makundi yako, nawe ulibadilisha ujira wangu mara kumi. 42Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hakuwa pamoja nami, hakika ungenifukuza mikono mitupu. Lakini Mungu ameona taabu yangu na kazi ngumu ya mikono yangu, naye usiku uliopita amekukemea.”
43Labani akamjibu Yakobo, “Wanawake hawa ni binti zangu, watoto hawa ni watoto wangu, na makundi haya ni makundi yangu. Vyote unavyoviona ni vyangu. Lakini hata hivyo ninaweza kufanya nini kuhusu hawa binti zangu, au kuhusu watoto waliowazaa? 44Njoo sasa na tufanye agano, wewe na mimi, na liwe kama shahidi kati yetu.”
45Hivyo Yakobo akachukua jiwe, akalisimamisha kama nguzo. 46Akawaambia jamaa yake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kuyakusanya yakawa lundo; wakala chakula hapo karibu na hilo lundo. 47Labani akaliita Yegar-Sahadutha#31:47 maana yake Lundo la ushahidi kwa Kiaramu na Yakobo akaliita Galeedi.#31:47 maana yake Lundo la ushahidi kwa Kiebrania
48Labani akasema, “Lundo hili ni shahidi kati yako na mimi leo.” Ndiyo maana likaitwa Galeedi. 49Pia liliitwa Mispa#31:49 maana yake Mnara wa ulinzi, kwa sababu alisema, “Mwenyezi Mungu na aweke ulinzi kati yako na mimi wakati hatuko pamoja. 50Ukiwatenda mabaya binti zangu au ukioa wake wengine zaidi ya binti zangu, hata ingawa hakuna hata mmoja aliye pamoja nasi, kumbuka kwamba Mungu ni shahidi kati yako na mimi.”
51Pia Labani akamwambia Yakobo, “Hili ndilo lundo, na hii ndiyo nguzo niliyoisimamisha kati yako na mimi. 52Lundo hili ni shahidi na nguzo hii ni shahidi, kwamba sitavuka lundo hili kuja upande wako kukudhuru, nawe kwamba hutavuka lundo hili na nguzo hii kuja upande wangu kunidhuru. 53Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba zao, aamue kati yetu.”
Hivyo Yakobo akaapa kwa jina la Hofu ya baba yake Isaka. 54Yakobo akatoa dhabihu huko nchi ya vilima na akawaalika jamaa zake kula chakula. Baada ya kula, wakalala huko.
55Kesho yake asubuhi na mapema, Labani akawabusu wajukuu zake na binti zake, na kuwabariki. Kisha akaondoka, akarudi nyumbani.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 31: ONMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia