Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 26

26
Isaka na Abimeleki
1Basi njaa kubwa ikatokea katika nchi hiyo, mbali na njaa iliyotokea wakati wa Ibrahimu. Isaka akaenda kwa Abimeleki mfalme wa Wafilisti huko Gerari. 2Mwenyezi Mungu akamtokea Isaka, akamwambia, “Usiende Misri, bali ukae katika nchi nitakayokuambia. 3Kaa katika nchi hii kwa kitambo; mimi nitakuwa pamoja na wewe na nitakubariki. Kwa maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote, na nitatimiza kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. 4Nitafanya wazao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa nchi hizi zote, na kupitia uzao wako mataifa yote yatabarikiwa, 5kwa sababu Ibrahimu alinitii mimi, na akatenda yote niliyomwagiza, akahifadhi amri zangu, na hukumu zangu, pamoja na sheria zangu.” 6Hivyo Isaka akaishi huko Gerari.
7Wanaume wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Wanaume wa huku wanaweza kuniua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa ni mzuri wa sura.”
8Isaka alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona Isaka akimpapasa Rebeka, mke wake. 9Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu’?”
Isaka akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”
10Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotutendea? Ingewezekana mtu yeyote akakutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia kwetu.”
11Hivyo Abimeleki akatoa amri kwa watu wote, akisema, “Yeyote atakayemnyanyasa mtu huyu au mkewe hakika atauawa.”
12Isaka akapanda mazao katika nchi hiyo, na kwa mwaka huo huo akavuna mara mia, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimbariki. 13Isaka akawa tajiri, nayo mali yake ikaendelea kuongezeka hata akawa tajiri sana. 14Akawa na mifugo ya kondoo na ng’ombe, na watumishi wengi sana, kiasi kwamba Wafilisti wakamwonea wivu. 15Kwa hiyo visima vyote vilivyochimbwa na watumishi wakati wa Ibrahimu baba yake, Wafilisti wakavifukia, wakavijaza udongo.
16Ndipo Abimeleki akamwambia Isaka, “Ondoka kwetu, kwa maana umetuzidi nguvu sana.”
17Basi Isaka akatoka huko, akajenga kambi katika Bonde la Gerari, akaishi huko. 18Ndipo Isaka akavichimbua tena vile visima vya maji ambavyo vilichimbwa siku zile za Ibrahimu baba yake, ambavyo Wafilisti walivifukia baada ya Ibrahimu kufa, akavipa majina yale yale ambayo baba yake alikuwa amevipa.
19Watumishi wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakagundua huko kisima chenye maji safi. 20Lakini wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, “Maji haya ni yetu!” Ndipo akakiita kile kisima Eseki#26:20 maana yake Ugomvi, kwa sababu waligombana naye. 21Kisha wakachimba kisima kingine, lakini hata hicho pia wakakigombania; akakiita Sitna#26:21 maana yake Upinzani. 22Akaondoka huko, akachimba kisima kingine, wala hakuna yeyote aliyekigombania. Akakiita Rehobothi#26:22 maana yake Mungu ametufanyia nafasi, akisema, “Sasa Mwenyezi Mungu ametufanyia nafasi, nasi tutastawi katika nchi.”
23Kutoka pale akaenda Beer-Sheba. 24Usiku ule Mwenyezi Mungu akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa Ibrahimu baba yako. Usiogope, kwa maana mimi niko pamoja nawe. Nitakubariki na kuongeza idadi ya wazao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.”
25Isaka akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Mwenyezi Mungu. Akapiga hema lake huko, nao watumishi wake wakachimba kisima.
26Wakati huo, Abimeleki alikuwa amemjia kutoka Gerari, akifuatana na Ahuzathi mshauri wake, pamoja na Fikoli jemadari wa majeshi yake. 27Isaka akawauliza, “Mbona mmekuja kwangu, na ninyi mlinichukia na kunifukuza?”
28Wakamjibu, “Tuliona wazi kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja nawe, kwa hiyo tukasema, ‘Inabidi kuwe na kiapo cha mapatano kati yetu,’ yaani kati yetu na wewe. Na tufanye mkataba pamoja nawe, 29kwamba hutatudhuru, kama vile nasi hatukuwanyanyasa bali tuliwatendea mema wakati wote, na tukawaaga kwa amani. Tena sasa umebarikiwa na Mwenyezi Mungu.”
30Basi Isaka akawaandalia karamu, nao wakala na kunywa. 31Kesho yake asubuhi na mapema wakaapiana. Kisha Isaka akawaruhusu waende zao, wakamwacha kwa amani.
32Siku hiyo watumishi wa Isaka wakaja, wakampa habari kuhusu kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, “Tumepata maji!” 33Naye akakiita Shiba#26:33 maana yake Saba au Kiapo; hadi leo mji huo unaitwa Beer-Sheba#26:33 maana yake Kisima cha saba au Kisima cha kiapo.
34Esau alipokuwa na umri wa miaka arobaini, akamwoa Yudithi binti Beeri Mhiti, kisha akamwoa Basemathi binti Eloni Mhiti. 35Hawa walikuwa chanzo cha huzuni kwa Isaka na Rebeka.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 26: ONMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia