Mwanzo 21
21
Kuzaliwa kwa Isaka
1Wakati huu Mwenyezi Mungu akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, na Mwenyezi Mungu akamtendea Sara kama alivyoahidi. 2Sara akapata mimba, na akamzalia Ibrahimu mwana katika uzee wake, katika majira yale Mungu alikuwa amemwahidi. 3Ibrahimu akampa huyo mwana ambaye Sara alimzalia jina Isaka#21:3 maana yake Kicheko au Anacheka. 4Isaka alipokuwa na umri wa siku nane, Ibrahimu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru. 5Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka mia moja Isaka mwanawe alipozaliwa.
6Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, na kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.” 7Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Ibrahimu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Lakini nimemzalia mwana katika uzee wake.”
Hajiri na Ishmaeli wafukuzwa
8Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya. Siku ile Isaka aliyoachishwa kunyonya, Ibrahimu alifanya sherehe kubwa. 9Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hajiri Mmisri alimzalia Ibrahimu alikuwa anadhihaki. 10Hivyo Sara akamwambia Ibrahimu, “Mwondoe mjakazi huyu mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mjakazi huyo kamwe hatarithi na mwanangu Isaka.”
11Jambo hili lilimhuzunisha sana Ibrahimu kwa sababu lilimhusu mwanawe. 12Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana huyo na mjakazi wako. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka. 13Nitamfanya huyu mwana wa mjakazi wako kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
14Kesho yake asubuhi na mapema, Ibrahimu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hajiri. Akaviweka begani mwa Hajiri, akamwondoa pamoja na kijana. Hajiri akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
15Maji yalipokwisha kwenye kiriba, Hajiri akamwacha kijana chini ya kichaka. 16Kisha akaenda akaketi kama umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Akiwa ameketi pale, akaanza kulia kwa huzuni.
17Mungu akamsikia kijana akilia. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini, Hajiri? Usiogope, Mungu amesikia kijana akilia akiwa amelala pale. 18Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19Ndipo Mungu akamfumbua Hajiri macho, akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
20Mungu akawa pamoja na huyo kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde. 21Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akamtwalia mke kutoka Misri.
Mapatano katika Beer-Sheba
22Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Ibrahimu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
24Ibrahimu akasema, “Ninaapa hivyo.”
25Ndipo Ibrahimu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyang’anya. 26Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ametenda hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
27Hivyo Ibrahimu akaleta kondoo na ng’ombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano. 28Ibrahimu akatenga kondoo jike saba kutoka kwa kundi. 29Abimeleki akamuuliza Ibrahimu, “Ni nini maana ya hawa kondoo jike saba uliowatenga peke yao?”
30Ibrahimu akamjibu, “Pokea hawa kondoo jike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
31Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu hao wawili waliapiana hapo.
32Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi nchi ya Wafilisti. 33Ibrahimu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa milele. 34Naye Ibrahimu akakaa nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 21: ONMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.