Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 18

18
Wageni watatu
1Mwenyezi Mungu akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. 2Ibrahimu akainua macho, akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, akaharakisha kutoka ingilio la hema lake, akawalaki na kusujudu hadi chini.
3Ibrahimu akasema, “Bwana wangu, ikiwa nimepata kibali machoni mwako, usimpite mtumishi wako. 4Acha yaletwe maji kidogo, nanyi mnawe miguu yenu, na mpumzike chini ya mti huu. 5Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.”
Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”
6Hivyo Ibrahimu akaharakisha akaingia kwenye hema kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”
7Kisha Ibrahimu akakimbia kwenye kundi, akachagua ndama mzuri laini, na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.
9Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?”
Akasema, “Yuko ndani ya hema.”
10Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Hakika nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, na Sara mkeo atakuwa na mwana.”
Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema lililokuwa nyuma ya Ibrahimu. 11Ibrahimu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amepita umri wa kuzaa mtoto. 12Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”
13Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu? Nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, naye Sara atakuwa na mwana.”
15Sara akaogopa, hivyo akadanganya na kusema, “Mimi sikucheka.”
Lakini Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, ulicheka!”
Ibrahimu aiombea Sodoma
16Watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, naye Ibrahimu akatembea nao ili awasindikize. 17Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Je, nimfiche Ibrahimu jambo ninalokusudia kufanya? 18Hakika Ibrahimu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, na kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. 19Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Mwenyezi Mungu atimize ahadi yake kwa Ibrahimu.”
20Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi zao zinanisikitisha sana, 21hivyo nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”
22Basi wale watu wakageuka, wakaelekea Sodoma, lakini Ibrahimu akabaki amesimama mbele za Mwenyezi Mungu. 23Ibrahimu akamsogelea, akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24Je, ikiwa watakuwepo watu hamsini wenye haki katika mji huo, kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo? 25Na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo: kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Liwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya haki?”
26Mwenyezi Mungu akajibu, “Nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitauacha huo mji wote kwa ajili yao.”
27Kisha Ibrahimu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu. 28Je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”
Bwana akamjibu, “Nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”
29Ibrahimu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”
Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”
30Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”
Akajibu, “Sitauangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”
31Ibrahimu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, wakipatikana huko watu ishirini tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”
32Ibrahimu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”
33Mwenyezi Mungu alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, akaondoka, naye Ibrahimu akarudi nyumbani.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 18: ONMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia