Mwanzo 16
16
Hajiri na Ishmaeli
1Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mjakazi Mmisri jina lake Hajiri. 2Hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Mwenyezi Mungu amenizuilia kupata watoto. Basi nenda ukutane kimwili na mjakazi wangu; huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”
Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. 3Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mjakazi wake Mmisri aliyeitwa Hajiri, na kumpa mumewe awe mke wake. 4Abramu akakutana kimwili na Hajiri, naye akapata mimba.
Hajiri alipojua kuwa ana mimba, akaanza kumdharau Sarai. 5Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na mateso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mkononi mwako. Sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Mwenyezi Mungu na aamue kati yako na mimi!”
6Abramu akamwambia, “Haya, mtumishi wako yuko mkononi mwako. Mtendee lolote utakalo!” Ndipo Sarai akamtesa Hajiri, naye akamtoroka.
7Malaika wa Mwenyezi Mungu akamkuta Hajiri karibu na chemchemi huko jangwani; chemchemi hiyo ilikuwa kando ya barabara iendayo Shuri. 8Malaika akamwambia, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi, na unaenda wapi?”
Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”
9Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” 10Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”
11Pia malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia:
“Wewe sasa una mimba
nawe utamzaa mwana.
Utamwita jina lake Ishmaeli#16:11 maana yake Mungu husikia,
kwa sababu Mwenyezi Mungu amesikia kuhusu huzuni yako.
12Atakuwa kama punda-mwitu kati ya wanadamu;
mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu,
na mkono wa kila mtu utakuwa dhidi yake,
naye ataishi kwa uhasama
na ndugu zake wote.”
13Hajiri akampa Mwenyezi Mungu aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” 14Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi#16:14 maana yake Yeye Aliye Hai Anionaye; bado kipo hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.
15Hivyo Hajiri akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hajiri aliyemzalia jina la Ishmaeli. 16Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita Hajiri alipomzalia Ishmaeli.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 16: ONMM
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.