Yobu 41
41
1“Yeyote anayeliona hilo dude,
hufa moyo na kuzirai.
2Hakuna mtu yeyote mkali athubutuye kulishtua.
Nani, basi awezaye kusimama mbele yangu?
3Nani aliyenipa kitu, ili nitakiwe kumrudishia?
Chochote kilicho chini ya mbingu ni changu.#41:3 maana katika makala ya Kiebrania si dhahiri.
4“Sitaacha kukueleza juu ya viungo vya hilo dude
au juu ya nguvu zake na umbo lake zuri.
5Nani awezaye kumbambua vazi lake la nje?
Nani awezaye kutoboa deraya lililovaa?
6Nani awezaye kufungua kinywa chake?
Meno yake pande zote ni kitisho!
7Mgongo#41:7 Mgongo; kadiri ya Septuaginta: Makala ya Kiebrania: Fahari. wake umefanywa kwa safu za ngao
zilizoshikamana pamoja kama kwa mhuri,
8Kila moja imeshikamana na nyingine,
hata hewa haiwezi kupenya katikati yake.
9Yameunganishwa pamoja,
hata haiwezekani kuyatenganisha.
10Likipiga chafya, mwanga huchomoza,
macho yake humetameta kama jua lichomozapo.
11Kinywani mwake hutoka mienge iwakayo,
cheche za moto huruka nje.
12Puani mwake hufuka moshi,
kama vile chungu kinachochemka;
kama vile magugu yawakayo.
13Pumzi yake huwasha makaa;
mwali wa moto hutoka kinywani mwake.
14Shingo yake ina nguvu ajabu,
litokeapo watu hukumbwa na hofu.
15Misuli yake imeshikamana pamoja,
imara kama chuma wala haitikisiki.
16Moyo wake ni mgumu kama jiwe,
mgumu kama jiwe la kusagia.
17Linapoinuka, mashujaa hushikwa na woga,
kwa pigo moja huwa wamezirai.
18Hakuna upanga uwezao kulijeruhi,
wala mkuki, mshale au fumo.
19Kwake chuma ni laini kama unyasi,
na shaba kama mti uliooza.
20Mshale hauwezi kulifanya likimbie;
akitupiwa mawe ya teo huyaona kama makapi.
21Kwake, rungu ni kama kipande cha bua,
hucheka likitupiwa fumo kwa wingi.
22Tumbo lake ni kama limefunikwa na vigae vikali;
hukwaruza na kurarua udongo kama chombo cha kupuria.
23Bahari huisukasuka kama maji yachemkayo,
huifanya itoe povu kama chupa ya mafuta.
24Lipitapo huacha nyuma alama inayongaa;
povu jeupe huonekana limeelea baharini.
25Duniani hakuna kinachofanana nalo;
hilo ni kiumbe kisicho na hofu.
26Huwaona kuwa si kitu wote wenye kiburi;
hilo ni mfalme wa wanyama wote wakali.”
Iliyochaguliwa sasa
Yobu 41: BHND
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jifunze Mengi Kuhusu Biblia Habari Njema