Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 39

39
1“Je, wajua mbuzi wa milimani huzaa lini,
au umewahi kuona kulungu akizaa?
2Je, wajua huchukua mimba kwa muda gani,
au siku yenyewe ya kuzaa waijua?
3“Wajua wakati watakapochuchumaa kuzaa,
wakati wa kuzaa watoto wao?
4Watoto wao hupata nguvu,
hukua hukohuko porini,
kisha huwaacha mama zao na kwenda zao.
5“Nani aliyemwacha huru pundamwitu?
Nani aliyewaacha waende kwa kuwafungua?
6Mimi niliwapa jangwa liwe makao yao,
mbuga zenye chumvi kuwa makazi yao.
7Hujitenga kabisa na makelele ya miji,
hasikilizi kelele ya kumfanyisha kazi.
8Hutembeatembea milimani kupata malisho,
na kutafuta chochote kilicho kibichi.
9“Je, nyati atakubali kukutumikia?
Au je, atakubali kulala zizini mwako?
10Je, waweza kumfunga nyati kamba kulima shamba,
au avute jembe la kulimia?
11Je, utamtegemea kwa kuwa ana nguvu nyingi
na kumwacha akufanyie kazi zako nzito?
12Je, wamtazamia nyati akuvunie mavuno yako,
na kuleta nafaka mahali pa kupuria?
13“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa madaha,
lakini hawezi kuruka kama korongo.#39:13 aya hii katika Kiebrania si dhahiri.
14Mbuni huyaacha mayai yake juu ya ardhi
ili yapate joto mchangani;
15lakini hajui kama yanaweza kukanyagwa,
au kuvunjwa na mnyama wa porini.
16Mbuni huwatendea wanawe ukatili kama si wake,
hata kazi yake ikiharibika yeye hana wasiwasi;
17kwa sababu nilimfanya asahau hekima yake,
wala sikumpa sehemu yoyote ya akili.
18Lakini akianza kukimbia,
humcheka hata farasi na mpandafarasi.
19“Je, Yobu, ndiwe uliyewapa farasi nguvu,
ukawavika shingoni manyoya marefu?
20Je, ni wewe unayemfanya farasi aruke kama nzige?
Mlio wake wa maringo ni wa ajabu!
21Huparapara ardhi mabondeni kwa pupa;
hukimbilia kwenye mapigano kwa nguvu zake zote.
22Farasi huicheka hofu, na hatishiki;
wala upanga hauwezi kumrudisha nyuma.
23Silaha wachukuazo wapandafarasi,
hugongana kwa sauti na kungaa juani.
24Farasi husonga mbele, akitetemeka kwa hasira;
tarumbeta iliapo, yeye hasimami.
25Kila ipigwapo tarumbeta, yeye hutoa sauti;
huisikia harufu ya vita toka mbali,
huusikia mshindo wa makamanda
wakitoa amri kwa makelele.
26“Je, mwewe amejifunza kwako jinsi ya kuruka,
na kunyosha mabawa yake kuelekea kusini?
27Je, tai hupaa juu kwa amri yako,
na kuweka kiota chake juu milimani?
28Tai hufanya makazi yake juu ya miamba mirefu,
na ncha kali za majabali ndizo ngome zake.
29Kutoka huko huotea mawindo,
macho yake huyaona kutoka mbali.
30 # Taz Mat 24:28; Luka 17:37 Makinda yake hufyonza damu;
pale ulipo mzoga ndipo alipo tai.”

Iliyochaguliwa sasa

Yobu 39: BHND

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia