Danieli na Makuhani wa Beli 1
1
1Baada ya kifo cha mfalme Astiage, Koreshi, Mpersi, alishika ufalme. 2Danieli alikuwa rafiki mwandani wa mfalme naye mfalme alimheshimu kuliko wenzake wote.
3Basi, Wababuloni walikuwa na sanamu ya mungu aitwaye Beli; kila siku waliitolea tambiko: Pishi kumi na mbili za nafaka, kondoo arubaini na lita 240 za divai. 4Mfalme Koreshi aliiheshimu sanamu hiyo, akawa anakwenda kuiabudu kila siku. Lakini Danieli alimwabudu Mungu wake binafsi.
5Basi, siku moja, mfalme akamwuliza Danieli, “Kwa nini humwabudu Beli?” Danieli akamjibu, “Mimi siabudu sanamu ambazo zimetengenezwa na watu. Mimi namwabudu Mungu aliye hai, Mungu Muumba wa mbingu na dunia na mwenye mamlaka juu ya wanaadamu wote.”
6Hapo, mfalme akamwambia Danieli, “Je, wewe huamini kwamba Beli ni mungu wetu aliye hai? Huoni jinsi anavyokula na kunywa kwa wingi kila siku?” 7Danieli akacheka na kumwambia mfalme, “Ewe mfalme, usidanganyike! Mungu huyo ni udongo ndani na shaba nje; hali wala hanywi chochote!”
8Hapo, mfalme alikasirika, akawaita makuhani wake, akawaambia, “Msiponiambia ni nani anayekula vyakula vyote hivyo mtakufa! 9Lakini mkinihakikishia kwamba Beli ndiye anayevila, basi, Danieli atauawa, kwa sababu amemkufuru Beli.” Naye Danieli akamwambia mfalme, “Sawa; na iwe kama ulivyosema!”
10Basi, mfalme akaingia ndani ya hekalu la Beli pamoja na Danieli. Humo ndani mlikuwa na makuhani sabini wa Beli, pamoja na wake zao na watoto wao. 11Makuhani hao wakamwambia mfalme, “Sasa, sisi tutatoka nje. Nawe, ee mfalme, mwandalie Beli chakula na kumwekea gudulia la divai, kisha ufunge mlango kabisa na kuweka mhuri kwa pete yako mwenyewe. 12Ukifika kesho asubuhi ukakuta kwamba Beli hajala kila kitu, basi, hapo na tuuawe; la sivyo, itamlazimu Danieli auawe, kwa sababu ametusingizia bure.” 13Makuhani hawakuwa na wasiwasi, maana chini ya meza walikuwa wameweka mlango wa siri waliopitia kila mara na kula vyakula hivyo.
14Basi, makuhani wakatoka nje, naye mfalme akamwandalia Beli vyakula. Kisha, Danieli akaamuru watumishi wake walete majivu na kuyanyunyizia kila mahali hekaluni, bila mtu mwingine kujua isipokuwa mfalme peke yake. Kisha wakatoka nje, wakaufunga mlango na kuutia mhuri kwa pete ya mfalme; kisha wakaenda zao.
15Usiku, kama ilivyokuwa kawaida yao, wale makuhani walikuja pamoja na wake zao na watoto wao, wakala chakula chote na kunywa divai yote.
16Mapema kesho yake asubuhi, mfalme akaenda hekaluni pamoja na Danieli. 17Basi, mfalme akamwuliza Danieli, “Je, mihuri iko sawasawa?” Danieli akajibu, “Naam, mfalme; iko sawasawa.” 18Mara tu mlango ulipofunguliwa, mfalme aliitazama meza tupu mbele ya Beli, akapaaza sauti, “Wewe u mkuu ewe Beli! Kwako hamna udanganyifu, hamna hata kidogo!” 19Lakini Danieli akaangua kicheko, na kumzuia mfalme asiingie ndani. Kisha akamwambia, “Hebu tazama sakafuni, mfalme! Nyayo hizo zote ni za kina nani?” 20Mfalme akasema, “Naam, naona nyayo za wanaume, wanawake na watoto.”
21Basi, mfalme hasira zikampanda, akaamuru makuhani na jamaa zao wote wakamatwe na kuletwa kwake. Nao wakamwonyesha milango ya siri waliyozoea kuingilia ndani kula vyakula vilivyowekwa mezani. 22Basi, mfalme akaamuru wauawe; na ile sanamu ya Beli akamwachia Danieli, naye akaivunjavunja pamoja na hekalu lake.
Danieli anaua Joka
23Wababuloni vilevile waliiabudu joka moja kubwa sana. 24Siku moja, mfalme akamwambia Danieli, “Huwezi kukana kuwa huyu si mungu hai. Kwa hiyo mwabudu!” 25Danieli akasema, “Mimi humwabudu Bwana Mungu wangu; yeye peke yake ndiye Mungu aliye hai. 26Kama wewe mfalme utaniruhusu, mimi nitaliua hilo joka bila kutumia panga wala rungu.” Mfalme akamwambia, “Haya! Nakuruhusu!”
27Basi, Danieli akachukua lami, mafuta na nywele, akavitokosa pamoja na kufanya donge, akalitupia mdomoni joka hilo, nalo likameza; ghafla likapasuka. Hapo Danieli akasema, “Haya! Liangalieni joka hilo ambalo mmekuwa mkiliabudu!”
28Wababuloni walipoona jambo hilo, walifanya maandamano ya hasira dhidi ya mfalme, wakapaaza sauti wakisema, “Mfalme amekuwa Myahudi! Yeye alimwangamiza Beli na makuhani akawachinja! Na sasa ameliua joka letu.” 29Basi, wakamwendea mfalme, wakasema, “Tutolee huyo Danieli! La sivyo, tutakuua pamoja na jamaa yako!” 30Mfalme alipoona kwamba wamembana sana na kumshurutisha, akamkabidhi Danieli kwao.
Danieli katika pango la simba
31Basi, wakamchukua Danieli na kumtumbukiza ndani ya pango la simba, naye akakaa humo kwa muda wa siku sita. 32Humo pangoni mlikuwa na simba saba ambao kwa desturi walikuwa wanalishwa binadamu wawili na kondoo wawili kila siku. Kwa muda wa siku sita, simba hao hawakupewa chochote ili wamtafune Danieli mara moja.
33Wakati huo, nabii Habakuki alikuwa huko Yuda. Basi, Habakuki alikuwa amepika mchuzi na mkate, akaviweka ndani ya bakuli, na akawa anakwenda shambani kuwapelekea wavunaji. 34Lakini, malaika wa Bwana akamwambia Habakuki, “Peleka chakula hicho Babuloni, kwa Danieli aliye katika pango la simba.” 35Habakuki akasema, “Bwana, mimi sijapata kufika Babuloni, wala sijui chochote kuhusu pango hilo.” 36Hapo malaika wa Bwana akamshika Habakuki nywele, akamnyanyua na kumpeleka kasi kwa upepo hadi Babuloni. Kisha akamweka palepale ukingoni mwa pango la hao simba.
37Basi, Habakuki akapaaza sauti, “Danieli! Danieli! Chukua chakula ambacho Mungu amekuletea.” 38Danieli akasema, “Ee Mungu, kweli umenikumbuka! Wewe kamwe huwaachi watu wakupendao katika taabu.” 39Basi, Danieli akainuka, akala. Malaika wa Bwana akamrudisha Habakuki nyumbani kwake.
40Mnamo siku ya saba, mfalme alikwenda kwenye pango la simba kumwombolezea Danieli. Lakini alipofika na kuchungulia ndani, alimwona Danieli ameketi, salama salimini. 41Mfalme akapaaza sauti na kusema, “Ee Bwana, Mungu wa Danieli! Wewe ni mkuu, na hakuna Mungu mwingine ila wewe!” 42Basi, akamtoa Danieli mle pangoni, na badala yake akawatupa ndani wale waliokuwa wanataka kumuua Danieli. Mara, wakararuliwa na simba na kuliwa mara moja, mfalme akiwa anatazama.
Iliyochaguliwa sasa
Danieli na Makuhani wa Beli 1: BHND
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jifunze Mengi Kuhusu Biblia Habari Njema