2 Wamakabayo 6
6
Wayahudi wadhulumiwa kwa sababu ya imani yao
1Baada ya muda si mrefu, mfalme alimtuma mzee mmoja Mwathene kuwashurutisha Wayahudi kuachilia mbali dini yao na mila na desturi za wazee wao. 2Pia aliagizwa kulitia najisi hekalu lao na kuliita “Hekalu la Zeu,” mungu wa Olimpia. Hekalu lililokuwa juu ya mlima Gerizimu ilibidi liitwe rasmi “Hekalu la Zeus, Mungu wa Ukarimu”, kama wakazi wa huko walivyoomba liitwe.
3Uovu uliofuata ulikuwa mbaya na wa kuchukiza mno. 4Watu wa mataifa mengine walilijaza hekalu kwa tafrija mbalimbali na kila aina ya ufisadi. Hata makahaba walitembea nao hekaluni. Vitu vilivyokatazwa viliingizwa hekaluni, 5na madhabahu ilifunikwa na tambiko za kuchukiza zilizokatazwa na sheria yetu. 6Haikuwezekana kuishika Sabato, wala kuadhimisha sikukuu za jadi, wala hata kujitaja waziwazi kuwa ni Myahudi. 7Kila mwezi ilipoadhimishwa siku ya kuzaliwa kwa mfalme, Wayahudi walilazimishwa kwa nguvu kula matumbo ya wanyama wa tambiko. Halafu, wakati wa sikukuu ya Dionisio, mungu wa divai, walitakiwa wavae mataji ya majani vichwani na kufanya maandamano. 8Kwa dokezo la Tolemai, miji ya Kigiriki ya jirani pia iliagizwa kuwataka Wayahudi wale tambiko; 9na wote ambao wangekataa kuishi kadiri ya utamaduni wa Kigiriki, iliamuriwa wauawe. Haikuwa vigumu kuona kwamba wakati mgumu ulikuwa unakuja. 10Mathalani, wanawake wawili walishikwa kwa sababu waliwatahiri watoto wao. Walitembezwa kuzunguka mji huku watoto wao wananing'inia kwenye maziwa yao; halafu wakatupwa chini kutoka ukuta wa mji. 11Tukio jingine. Filipo aliambiwa kwamba Wayahudi kadha walikuwa wamekusanyika katika pango la karibu ili kushika Sabato kwa siri. Filipo akawashambulia na kuwachoma moto wote pamoja. Wao lakini hawakujitetea kwa mabavu, kwa vile waliiheshimu sana Sabato.
Bwana huadhibu na kuhurumia
12Hapa nawahimiza wasomaji wa makala haya wasivunjike moyo kutokana na misiba ya kutisha iliyotukia. Ieleweke kwamba adhabu hizo zilitolewa na Bwana siyo kuwaangamiza bali kuwapa nidhamu. 13Kwa kweli, kumwadhibu mtu mpotovu ni ishara ya huruma kubwa, kuliko kumwachilia kwa muda mrefu bila adhabu. 14Bwana hatutendei sisi kama anavyoyatendea mataifa mengine. Hao wengine huwaadhibu baada ya kungoja kwa uvumilivu mpaka wamezama kabisa dhambini; 15lakini sisi hutuadhibu kabla hatujatenda dhambi mno. 16Kwa hiyo, Bwana anatuhurumia daima, sisi watu wake. Ingawa hutuadhibu kwa misiba, kamwe hatutupi. 17Nimeeleza hayo machache kwa kuwakumbusheni tu. Sasa tuendelee na simulizi letu.
Eleazari afia imani yake
18Palikuwa na mwalimu mmoja wa sheria aitwaye Eleazari, mtu mzee na mwenye kuheshimiwa sana. Huyo alifunguliwa mdomo wake kwa nguvu kula nyama ya nguruwe. 19Lakini Eleazari aliona heri kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa upotovu. Basi, akatema hiyo nyama na kwenda kwa hiari yake mahali pa kuteswa, 20akionesha jinsi watu wanavyopaswa kuwa wajasiri kukataa kula chakula najisi, hata kama kufanya hivyo kutawagharimu maisha yao. 21Watu waliohusika na tambiko hiyo walikuwa wanamjia Eleazari sana, hivyo walimchukua kando, wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali kuliwa, ajifanye kana kwamba anakula nyama ya tambiko ambayo mfalme aliamuru itolewe. 22Kwa kufanya hivyo hangeuawa, na angetendewa vizuri kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani.
23Lakini Eleazari akakata shauri lililostahili mtu mzee na umri wake mkubwa. Tangu utoto wake alikuwa ameishi kwa kushika kikamilifu amri takatifu za Mungu. Hivyo akajibu: “Niueni, hapahapa, sasa hivi. 24Mtu wa umri mkubwa kama wangu, ni aibu kudanganya namna hiyo. Vijana wengi wasije wakafikiri kwamba nimeikana imani yangu baada ya kutimiza umri wa miaka tisini. 25Kama nitafanya kana kwamba nakula nyama hii, ili tu niendelee kuishi kidogo tena, nitakuwa nimejiletea aibu na fedheha, na vijana wengi watakuwa wamepotoshwa. 26Hata kama ningeweza kwa sasa kuepuka hilo pigo la watu wafao, sitaweza kuuepa mkono wa Mungu Mwenye Nguvu niwe hai au nimekufa. 27Kwa kukipokea kifo sasa kwa uhodari, nitadhihirisha kwamba nastahili uzee wangu. 28Hapo vijana watajifunza kutokana na mfano wangu, jinsi ipasavyo kukubali kwa furaha kufa kwa ajili ya sheria za kale na takatifu za Mungu.”
Alipokwisha sema hayo, alipaendea mahali pa kuteswa. 29Na watu walewale waliokuwa wamemfanyia kirafiki dakika chache kabla yake, sasa walimgeukia, maana walidhani alikuwa ameongea kama mwendawazimu. 30Walipokuwa wamempiga mpaka karibu na kufa, Eleazari akatoa mlio wa maumivu na kusema: “Bwana ajua yote. Anajua kwamba ningeweza kuwa nimeepuka mateso haya makali na kifo. Pia anajua kwamba nimevumilia hayo kwa furaha, kwa sababu namcha yeye.” 31Hivyo ndivyo Eleazari alivyokufa. Lakini kifo chake cha ujasiri kilikumbukwa na kuhesabiwa kuwa mfano mtukufu si na vijana tu, bali na taifa lake zima.
Iliyochaguliwa sasa
2 Wamakabayo 6: BHND
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Jifunze Mengi Kuhusu Biblia Habari Njema