Luka 24
24
Wanawake kaburini.
(1-12: Mat. 28:1-8; Mar. 16:1-8; Yoh. 20:1-13.)
1Siku ya kwanza ya juma wakaenda kaburini asubuhi na mapema wakichukua manukato, waliyoyatengeneza. 2Wakaliona lile jiwe, limekwisha fingirishwa na kutoka kaburini. 3Walipoingia, hawakuuona mwili wake Bwana Yesu. 4Ikawa, walipopotelewa na jambo hili, mara wakawatokea watu wawili waliovaa nguo zimulikazo. 5Kwa kuingiwa na woga, wakaziinamisha nyuso zao chini; ndipo, wale walipowaambia: Aliye hai mnamtafutiaje penye wafu? 6Hayumo humu, ila amefufuliwa. Kumbukeni, alivyowaambia alipokuwa bado huko Galilea 7akisema: Mwana wa mtu sharti atiwe mikononi mwa watu wakosaji, awambwe msalabani, kisha afufuke siku ya tatu!#Luk. 9:22; Mat. 17:22-23. 8Ndipo, walipoyakumbuka hayo maneno yake, 9wakarudi toka kaburini, wakawasimulia wale kumi na mmoja na wengine wote haya yote. 10Nao walikuwa Maria Magadalene na Yohana na Maria, mama yake Yakobo, na wengine waliokuwa pamoja nao; hao ndio waliowapasha mitume habari hizi.#Luk. 8:2-3. 11Lakini wajapoyawazia maneno hayo kuwa upuzi tu, wasiwaitikie, 12Petero akainuka, akapiga mbio kufika kaburini, akainama, akachungulia, akaiona sanda tu. Kisha akaenda zake na kulistaajabu moyoni mwake lililokuwapo.
Wanafunzi wa Emao.
(13-35: Mar. 16:12-13.)
13*Siku ile wenzao wawili walikuwa wakienda, waje kijijini, jina lake Emao; mtu akitoka Yerusalemu, ni mwendo wa saa mbili. 14Nao walikuwa wakiongeana hayo yote yaliyokuwapo. 15Ikawa, wakiongea na kuulizana, Yesu mwenyewe akawakaribia, akaenda pamoja nao.#Mat. 18:20. 16Lakini macho yao yalikuwa, kama yamefumbwa, wasipate kumtambua. 17Alipowauliza: Ni maneno gani hayo, mnayoyaongea hapa njiani? wakasimama na kununa. 18Mmoja wao, jina lake Kleofa, akajibu akimwambia: Wewe u mgeni peke yako Yerusalemu, usiyatambue yaliyokuwamo siku hizi? 19Akawauliza: Yapi? Ndipo, walipomwambia: Mambo ya Yesu wa Nasareti! Alikuwa mfumbuaji mwenye nguvu ya kutenda na ya kusema mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.#Mat. 21:11. 20Huyo watambikaji wakuu na wakubwa wetu wamemtoa, ahukumiwe kuuawa, wakamwamba msalabani. 21Lakini sisi twalimngojea, ya kuwa ndiye atakayewakomboa Waisiraeli. Yakiisha hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu hapo, yalipokuwapo.#Tume. 1:6. 22Tena wako wanawake wa kwetu waliotushangaza; walikwenda kaburini asubuhi na mapema,#Luk. 24:1-11. 23wasiuone mwili wake, wakaja, wakasema: Tumetokewa na malaika waliosema: Yeye yu hai. 24Tena wako wenzetu waliokwenda kaburini, wakavikuta vivyo hivyo, kama wanawake walivyosema, lakini mwenyewe hawakumwona.#Luk. 24:12; Yoh. 20:3-10. 25Ndipo, alipowaambia: Nyie msiotambua mambo, mnayo mioyo inayokawia kuyategemea yote, Wafumbuaji waliyoyasema. 26Haikumpasa Kristo kuteswa hivyo, apate kuingia katika utukufu wake? 27Akaanzia kwa Mose na kwa Wafumbuaji wote, akawaeleza, aliyoandikiwa katika Maandiko yote.#5 Mose 18:15,18; Sh. 22; Yes. 53. 28Walipokikaribia kijiji, walichokiendea, akajitendekeza, kama anataka kwenda mbele. 29Lakini wakambembeleza sana wakisema: Fikia mwetu! kwani ni jioni, nalo jua limekwisha kuchwa. Basi, akaingia kufikia mwao. 30Ikawa, alipokaa chakulani pamoja nao, akautwaa mkate, akauombea, akaumega, akawagawia.#Luk. 22:19. 31Ndipo, macho yao yalipofumbuliwa, wakamtambua. Naye papo hapo alikuwa ametoweka machoni pao. 32Kisha wakaambiana: Mioyo yetu humu ndani haikuwa ikiwaka moto, aliposema nasi njiani na kutueleza maana ya Maandiko? 33Wakainuka saa ileile, wakarudi Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja nao waliokuwa pamoja nao, 34wamekusanyika na kusema: Bwana amefufuka kweli! Amemtokea Simoni!#1 Kor. 15:4-5. 35Nao wakawasimulia, waliyoyaona njiani, na jinsi walivyomtambua, alipoumega mkate.*
Yesu anawatokea mitume.
(36-49: Mar. 16:14-18; Yoh. 20:19-23; 1 Kor. 15:5.)
36Walipokuwa wakiongea hivyo, mwenyewe akaja kusimama katikati yao, akawaambia: Tengemaneni! 37Wakastuka kwa kuingiwa na woga, wakawaza, wameona mzimu.#Mat. 14:26. 38Akawaambia: Mbona mnahangaika hivyo? Tena kwa nini mawazo kama hayo yanawaingia mioyoni mwenu? 39Yatazameni maganja yangu na miguu yangu, mjue: Ni mimi mwenyewe! Nipapaseni, mwone! Kwani mzimu hanayo nyama ya mwili wala mifupa, kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. 40Alipokwisha kuyasema haya akawaonyesha maganja na miguu. 41Lakini walipokuwa hawajamtegemea bado kwa kufurahiwa na kwa kushangaa, akawauliza: Mnacho cha kula hapa? 42Ndipo, walipompa kipande cha samaki kilichokaangwa.#Yoh. 21:10. 43Akakitwaa, akakila mbele yao. 44Kisha akawaambia: Haya ndiyo maneno yangu, niliyowaambia nilipokuwapo bado kwenu, ya kwamba: Sharti yatimizwe yote, niliyoandikiwa katika Maonyo ya Mose na katika wafumbuaji na katika Mashangilio.#Luk. 9:22; 18:31-33; 24:27. 45Ndipo, alipowafumbua akili, waelewe na Maandiko. 46Akawaambia: Kwa hivyo vilivyoandikwa imempasa Kristo kuteswa na kufufuka katika wafu siku ya tatu; 47kisha wao wa mataifa yote watatangaziwa kwa Jina lake, wajute, wapate kuondolewa makosa; hivi vianzie Yerusalemu! 48Nanyi m mashahidi wa mambo haya.#Yoh. 15:26; 16:7; Tume. 1:4; 2:1. 49Mtaniona mimi, nikituma kwenu kiagio cha Baba yangu! Lakini kaeni tu mjini, mpaka mtakapotiwa nguvu itokayo juu!
Kupaa mbinguni.
(50-53: Mar. 16:19; Tume. 1:4-14.)
50*Kisha akatoka nao, akawapeleka mpaka Betania; hapo akaiinua mikono yake, akawabariki. 51Ikawa katika kuwabariki, akajitenga kwao akachukuliwa kwenda mbinguni.#Yoh. 3:13. 52Ndipo, walipomwangukia kifudifudi, kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu. 53Wakawapo hapo Patakatifu siku zote wakimtukuza Mungu.*
Iliyochaguliwa sasa
Luka 24: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.