Matendo ya Mitume 15
15
Mkutano wa mitume.
1Kulikuwa na watu waliotelemka toka Yudea, wakaja huko, wakawafundisha ndugu kwamba: Hamwezi kuokoka msipotahiriwa, kama Mose alivyotuzoeza.#Gal. 5:2. 2Ikawa, Paulo na Barnaba wakabishana nao kabisa na kushindana sana. Kisha wakamwagiza Paulo na Barnaba na wenzao wengine, wapande kwenda Yerusalemu kwao mitume na wazee kwa ajili ya mshindano huu.#Tume. 11:30; Gal. 2:1. 3Wakasindikizwa na wateule, wakapita Ufoniki na Samaria, wakaeleza Po pote, wamizimu walivyogeuka; hivyo wakawafurahisha sana ndugu wote. 4Walipofika Yerusalemu wakapokelewa nao wateule na mitume na wazee, wakayaeleza yote, Mungu aliyoyafanya kwa kuwa nao.#Tume. 14:27. 5Pakainuka waliokuwa wa chama cha Mafariseo, lakini nao walikuwa wenye kumtegemea Bwana, wakasema: Sharti watahiriwe! Sharti waagizwe kuyashika Maonyo ya Mose!
Shauri la Petero.
6Mitume na wazee wakakusanyika, walitazame neno hilo.#Tume. 10:44; 11:15. 7Mashindano yalipokuwa mengi, Petero akainuka, akawaambia: Waume ndugu, ninyi mnajua, ya kuwa siku zilizopita huku kwenu Mungu alikichagua kinywa changu, wamizimu wakisikie, kinavyowapigia hiyo mbiu njema, waje kuitegemea. 8Naye Mungu mwenye kuitambua mioyo akawapokea wamizimu alipowapa Roho Mtakatifu, kama alivyotupa na sisi. 9Tena hakuna, asichowalinganisha na sisi, maana nao amewang'aza mioyo kwa vile, walivyomtegemea.#Tume. 10:34. 10Sasa mwamjaribiaje Mungu mkiwatwisha wanafunzi mzigo, ambao baba zetu hawakuweza kuuchukua, uliotushinda nasi?#Gal. 3:10; 5:1. 11Lakini tunayategemea, ya kuwa tutaokolewa kwa kugawiwa na Bwana Yesu, sawasawa kama wale nao.#Gal. 2:16; Ef. 2:4-10. 12Basi, mkutano wote ukanyamaza, wakamsikiliza Barnaba na Paulo, wakivisimulia vielekezo na vioja vyote, Mungu alivyovifanya kwa mikono yao katika wamizimu.
Shauri la Yakobo.
13Waliponyamaza tena, Yakobo akajibu akisema: Waume ndugu, mnisikilize!#Tume. 21:18; Gal. 2:9. 14Simoni amesimulia, Mungu alivyoanza kuwachagua wamizimu, alipatie Jina lake kundi la watu humo namo.#Tume. 15:7-9. 15Nayo maneno ya Wafumbuaji huelekeza papo hapo, kama ilivyoandikwa kwamba:#Amo. 9:11-12.
16Hayo yakiisha, nitarudi, nikijenge tena
kibanda cha Dawidi kilichoanguka;
hapo palipojenguka nitapajenga tena, nipate kukisimamisha
tena,
17maana watu waliosalia wote wapate kumtafuta Bwana
pamoja na wamizimu wote waliotangaziwa Jina langu.
Ndivyo, asemavyo Bwana anayeyafanya haya.
18Yanatambulikana toka kale. 19Kwa hiyo mimi naona: Wanaotoka kwa wamizimu na kumgeukia Mungu tusiwachukuze mizigo isiyofaa, 20ila tuwaandikie kwamba: Miiko ni hii tu: Kutambikia mizimu, maana huchafua moyo wa mtu, tena ugoni, tena nyamafu, tena damu.#1 Mose 9:4; 3 Mose 3:17. 21Kwani toka kale hata sasa Mose anao mijini mote wanaoyatangaza maneno yake, tena katika nyumba za kuombea yanasomwa kila siku ya mapumziko.#Tume. 13:15.
Barua ya mitume.
22Ndipo, mitume na wazee walipopatana na wateule wote kuchagua wenzao wengineo na kuwatuma kwenda Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda anayeitwa Barsaba na Sila, waliojua kuongoza ndugu. 23Wakaandika barua, waipeleke mikononi mwao, ni ya kwamba: Sisi mitume na wazee tunawaamkia kindugu ninyi ndugu zetu huko Antiokia na Ushami na Kilikia mliotoka kwa wamizimu. 24Tumesikia, ya kuwa wengine watu, tusiowaagiza neno, wamewahangaisha kwa maneno ya kuwatia wasiwasi mioyoni mwenu.#Tume. 15:1. 25Tukakusanyika kwa hivyo, tulivyo na moyo mmoja, tukapatana kuchagua watu na kuwatuma kwenu pamoja na wenzetu akina Barnaba na Paulo, tunawapenda, 26kwani ni watu waliojitoka wenyewe kwa ajili ya Jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27Basi, tumemtuma Yuda na Sila, nao watawaelezea kwa vinywa maneno yaya haya. 28Kwani sisi na Roho Mtakatifu tumepatana, tusiwatwike mzigo kuliko yaleyale yanayofaa, 29mshike mzio wa nyama za tambiko na wa damu na wa nyamafu na wa ugoni. Mkijikataza mambo haya mtafanya vema. Kaeni vema! Salamu.
30Kisha wakasindikizwa, wakatelemka kwenda Antiokia, wakawakusanya wao wote wa hilo kundi, wakawatolea ile barua. 31Wale walipoisoma wakafurahi kwa ajili ya matulizo. 32Hata Yuda na Sila waliokuwa wafumbuaji wenyewe wakawatuliza ndugu na kuwaambia mengi, wakawashupaza.#Tume. 11:27; 13:1. 33Walipokwisha kukaa kitambo walisindikizwa na ndugu kwa hivyo, walivyopatana, warudi kwao waliowatuma. 34Lakini Sila alipendezwa kukaa huko. 35Naye Paulo na Barnaba wakakaa Antiokia wakilifundisha Neno la Bwana na kuipiga hiyo mbiu njema pamoja na wenzao wengi.
36Siku zilipopita, Paulo akamwambia Barnaba: Turudi tena, tuwakague ndugu mijini mote, tulimolitangaza Neno la Bwana!#1 Tes. 3:5. 37Lakini Barnaba alitaka kumchukua naye Yohana aliyeitwa Marko.#Tume. 12:12,25. 38Lakini Paulo alidhani, haifai kumchukua aliyewatoroka huko Pamfilia, asifuatane nao kazini.#Tume. 13:13. 39Kwa hiyo wakabishana kwa ukali, hata wakatengana yeye na mwenziwe; Barnaba akamchukua Marko, akaingia chomboni kwenda Kipuro, 40naye Paulo akamchukua Sila, akaondoka akiombewa na ndugu, Mungu awaongoze kwa upole. 41Akaipita nchi ya Ushami na Kilikia, akawashupaza wateule.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo ya Mitume 15: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.