Luka 20
20
Swali kuhusu mamlaka ya Yesu
1 #
Mt 21:23-27; Mk 11:27-33 Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri Habari Njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafla; 2wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka haya? 3Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni, 4Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? 5Wakaulizana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini? 6Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii. 7Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka. 8Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
Mfano wa wakodishaji shamba waovu
9 #
Mt 21:33-46; Mk 12:1-12 Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akakondisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. #Isa 5:1 10#2 Nya 36:15,16 Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. 11Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. 12Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. 13Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. 14Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. 15Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendaje? 16Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! 17#Zab 118:22 Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa,
Jiwe walilolikataa waashi,
Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni?
18 #
Isa 8:14
Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika; na yeyote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. 19#Lk 19:48 Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitaka kumkamata saa hiyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao.
Swali kuhusu kulipa kodi
20 #
Mt 22:15-22; Mk 12:13-17 Wakamviziavizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya mtawala. #Lk 11:54 21Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. 22Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? 23Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, 24Nionesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. 25Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. 26Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaza.
Swali kuhusu ufufuo
27 #
Mt 22:23-33,46; Mk 12:18-27,34 Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, #Mdo 23:8 28#Kum 25:5,6 wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. 29Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; 30na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] 31hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. 32Mwisho akafa yule mke naye. 33Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. 34Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; 35lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; 36#1 Yoh 3:1,2 wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. 37#Kut 3:2,6 Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura ya Kichaka, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. 38#Rum 14:8 Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa maana kwake wote wanaishi. 39Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; 40wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.
Suala kuhusu u-Wana wa Daudi
41 #
Mt 22:41-45; Mk 12:35-37 Akawaambia, Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? 42#Zab 110:1; Yn 7:42 Maana, Daudi mwenyewe asema katika kitabu cha Zaburi,
Bwana alimwambia Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kulia,
43Hadi niwaweke adui zako
Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako.
44Basi Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake?
Yesu awakana waandishi
45 #
Mt 23:1,5-7,14; Mk 12:38-40 Na watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake, #Lk 11:43 46Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni. 47Wanakula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo kuu.
Iliyochaguliwa sasa
Luka 20: RSUVDC
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013.