Mwanzo 19
19
Kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora
1Malaika wale wawili walifika Sodoma wakati wa jioni, naye Lutu alikuwa ameketi kwenye lango la mji. Alipowaona, alienda kuwalaki, akasujudu, uso wake ukagusa chini. 2Akasema, “Bwana zangu, tafadhali karibuni kwenye nyumba ya mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala hapa, kisha asubuhi na mapema mwendelee na safari yenu.”
Wakamjibu, “La, tutalala hapa uwanjani.”
3Lakini aliwasihi sana hadi wakaingia nyumbani mwake. Akawaandalia chakula, mikate isiyotiwa chachu, nao wakala. 4Kabla hawajaenda kulala, wanaume wote kutoka kila sehemu ya mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, waliizunguka nyumba. 5Wakamwita Lutu wakisema, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako jioni hii? Watoe nje kwetu ili tuwalawiti.”
6Lutu akatoka nje kuongea nao, akaufunga mlango nyuma yake. 7Akawaambia, “La hasha, rafiki zangu! Msifanye jambo hili ovu. 8Tazama, ninao binti zangu wawili ambao ni bikira. Acha niwatoe kwenu, nanyi mnaweza kuwafanyia lolote mnalotaka. Lakini msiwafanyie chochote wanaume hawa, kwa sababu wako chini ya ulinzi wa dari langu.”
9Wakamjibu, “Tuondokee mbali!” Wakaendelea kusema, “Huyu mtu alikuja hapa kama mgeni na sasa anataka kuwa mwamuzi wetu! Tutakutenda vibaya kuliko wao.” Waliendelea kumlazimisha Lutu na kuusogelea mlango ili kuuvunja.
10Lakini wanaume wale waliokuwa ndani wakanyoosha mikono yao, wakamvuta Lutu ndani ya nyumba na kuufunga mlango. 11Kisha wakawapiga kwa upofu wale wanaume waliokuwa mlangoni mwa ile nyumba, vijana kwa wazee, hivyo hawakuweza kuupata mlango.
12Wale wanaume wawili wakamwambia Lutu, “Una mtu mwingine yeyote hapa: wakwe, wana au binti, ama yeyote mwingine aliye wako katika mji huu? Waondoe hapa, 13kwa sababu tunapaangamiza mahali hapa. Kilio kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya watu wa hapa ni kikubwa kiasi kwamba ametutuma kupaangamiza.”
14Kwa hiyo Lutu alitoka ili kuzungumza na wakwe wake waliokuwa wamewaposa binti zake. Akawaambia, “Fanyeni haraka kuondoka mahali hapa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu yu karibu kuangamiza mji huu!” Lakini wakwe wake walifikiri kwamba alikuwa akitania.
15Kulipopambazuka, malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, “Fanya haraka! Mchukue mke wako na binti zako wawili walio huku, la sivyo utaangamizwa mji huu utakapoadhibiwa.”
16Alipositasita, wale wanaume wakamshika mkono wake, na mikono ya mke wake na binti zake wawili na kuwaongoza salama nje ya mji, kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwahurumia. 17Mara walipokwisha kuwatoa nje, mmoja wao akawaambia, “Mkimbie kwa usalama wenu! Msitazame nyuma, wala msisimame popote katika nchi tambarare! Kimbilieni milimani, ama sivyo mtaangamizwa!”
18Lakini Lutu akawajibu, “La hasha, bwana zangu, tafadhalini! 19Mtumishi wenu amepata kibali mbele ya macho yenu, nanyi mmeonesha wema mkubwa kwangu kwa kuokoa maisha yangu. Lakini siwezi kukimbilia milimani; janga hili litanikumba, nami nitakufa. 20Tazama, hapa kuna mji karibu wa kukimbilia, nao ni mdogo. Niruhusuni nikimbilie humo: Ni mdogo sana, ama sivyo? Ndipo maisha yangu yatasalimika.”
21Akamwambia, “Vema sana, nitalikubali hili ombi pia, sitauangamiza mji ulioutaja. 22Lakini ukimbilie huko haraka, kwa sababu sitaweza kufanya lolote hadi ufike huko.” (Ndiyo maana mji huo ukaitwa Soari#19:22 maana yake Mdogo.)
23Lutu alipofika Soari, jua lilikuwa limechomoza katika nchi. 24Ndipo Mwenyezi Mungu akanyesha moto wa kiberiti juu ya Sodoma na Gomora kutoka kwake Mwenyezi Mungu mbinguni. 25Hivyo akaiteketeza miji ile na eneo lote la tambarare, pamoja na wote walioishi katika miji hiyo, hata pia mimea yote katika nchi. 26Lakini mke wa Lutu akatazama nyuma, hivyo akawa nguzo ya chumvi.
27Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Ibrahimu akaamka na kurudi mahali pale aliposimama mbele za Mwenyezi Mungu. 28Akatazama upande wa Sodoma na Gomora, kuelekea nchi yote ya tambarare, akaona moshi mzito ukipanda kutoka nchi, kama moshi unaotoka katika tanuru.
29Kwa hiyo Mungu alipoiangamiza miji ya tambarare, alimkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu kutoka lile janga lililoharibu miji ile ambamo Lutu alikuwa ameishi.
Lutu na binti zake
30Lutu na binti zake wawili waliondoka Soari na kufanya makao yao kule milimani, kwa maana aliogopa kukaa Soari. Yeye na binti zake wawili waliishi katika pango. 31Siku moja binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanaume mahali hapa atakayekutana na sisi kimwili, kama ilivyo desturi ya mahali pote duniani. 32Tumnyweshe baba yetu mvinyo, kisha tukutane naye kimwili ili tuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.”
33Usiku ule walimnywesha baba yao mvinyo; alipolewa, binti yake mkubwa akaingia na kukutana naye kimwili. Baba yao hakujua binti yake alipoingia kulala naye wala alipotoka.
34Siku iliyofuata binti mkubwa akamwambia yule mdogo, “Usiku uliopita mimi nilikutana kimwili na baba yangu. Tumnyweshe divai tena, usiku huu nawe ukutane naye kimwili ili tuweze kuhifadhi uzao wetu kupitia baba yetu.” 35Kwa hiyo wakamnywesha baba yao mvinyo tena usiku ule, naye binti yake mdogo akaingia, akakutana naye kimwili. Kwa mara nyingine baba yao hakujua binti yake alipolala naye wala alipoondoka.
36Hivyo binti wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao. 37Binti mkubwa akamzaa mwana, akamwita jina Moabu#19:37 Kiebrania ni kama kusema Kutoka kwa baba.; ndiye baba wa Wamoabu hata leo. 38Binti mdogo pia akamzaa mwana, naye akamwita jina Benami#19:38 Kiebrania ni kama kusema Mwana wa jamaa ya baba.; ndiye baba wa Waamoni hata leo.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 19: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.