Mathayo 8
8
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mk 1:40-45; Lk 5:12-16)
1Yesu alipotelemka kutoka kwenye kilima, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 2Mtu mmoja mwenye ugonjwa unaogopewa sana wa ngozi akamwendea, akainama mbele yake mpaka chini na akasema, “Bwana ukitaka una uwezo wa kuniponya.”
3Yesu aliunyoosha mkono wake akamshika mtu yule mwenye ugonjwa hatari sana wa ngozi. Akasema, “Hakika, ninataka kukuponya. Upone!” Mtu huyo akapona ugonjwa hatari sana wa ngozi saa hiyo hiyo. 4Kisha Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea, lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.#8:4 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa (torati) ilisema kuhani ni lazima aamue ikiwa mtu amepona ugonjwa hatari wa ngozi. Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa wa Jeshi
(Lk 7:1-10; Yh 4:43-54)
5Yesu alikwenda Kapernaumu. Alipoingia mjini, afisa wa jeshi alimjia na kumwomba msaada. 6Akasema, “Bwana, mtumishi wangu ni mgonjwa sana nyumbani na amelala kitandani. Hawezi hata kutingishika na ana maumivu makali sana.”
7Yesu akamwambia yule afisa, “Nitakwenda nimponye.”
8Yule afisa akajibu, “Bwana, mimi si mwema kiasi cha wewe kuingia katika nyumba yangu. Toa amri tu, na mtumishi wangu atapona. 9Ninajua hii, kwa kuwa ninaelewa mamlaka. Kuna watu wenye mamlaka juu yangu, na nina askari walio chini ya mamlaka yangu. Nikimwambia askari mmoja ‘nenda’, huenda. Na nikimwambia mwingine ‘njoo’, huja. Pia nikimwambia mtumwa wangu ‘fanya hiki’, hunitii.”
10Yesu aliposikia maneno hayo alishangaa. Akawaambia wale waliokuwa wakifuatana naye, “Ukweli ni kuwa, mtu huyu ana imani kuliko mtu yeyote niliyewahi kumwona katika Israeli. 11Watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi na kula pamoja na Abrahamu, Isaka, na Yakobo katika ufalme wa Mungu. 12Na wale wanaopaswa kuwa katika ufalme watatupwa nje gizani. Na huko watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
13Kisha Yesu akamwambia yule afisa, “Rudi nyumbani kwako. Mtumishi wako atapona kama unavyoamini.” Mtumishi wa afisa huyo akapona wakati ule ule.
Yesu Amponya Mkwewe Petro
(Mk 1:29-31; Lk 4:38-39)
14Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa na homa. 15Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, kisha akasimama na kuanza kumhudumia.
Yesu Aponya Wengine Wengi
(Mk 1:32-34; Lk 4:40-41)
16Ilipofika jioni, watu wengi waliokaliwa na mashetani waliletwa kwa Yesu. Naye aliyaamuru mashetani hayo kuwaacha watu. Na aliowaponya wagonjwa wote. 17Hii ilitokea ili kutimiza maneno yaliyosemwa na nabii Isaya aliposema:
“Aliyaondoa magonjwa yetu
na kuyabeba madhaifu yetu.”#Isa 53:4
Kumfuata Yesu
(Lk 9:57-62)
18Yesu alipoona kundi la watu waliomzunguka, aliawaambia wafuasi waende upande mwingine wa ziwa. 19Kisha, mwalimu wa sheria ya Musa akamwendea na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kila mahali utakapokwenda.”
20Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo wanamoishi, ndege wana viota. Lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kupumzika.”
21Mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana mimi pia nitakufuata, lakini niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
22Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate mimi, na uwaache wale waliokufa wawazike wafu wao.”
Yesu Atuliza Dhoruba
(Mk 4:35-41; Lk 8:22-25)
23Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake. 24Baada ya mashua kutoka pwani, upepo wenye nguvu sana ukaanza kuvuma ziwani. Mawimbi yakaifunika mashua. Lakini Yesu alikuwa amelala. 25Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha. Wakamwambia, “Bwana tuokoe! Tutazama majini!”
26Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa? Hamna imani ya kutosha.” Yesu akasimama akaukemea upepo na mawimbi, na ziwa likatulia.
27Wanafunzi wake wakashangaa sana, wakasema, “Huyu ni mtu wa namna gani? Hata upepo na maji vinamtii!”
Yesu Afukuza Mashetani Kutoka Kwa Watu Wawili
(Mk 5:1-20; Lk 8:26-39)
28Yesu alifika ng'ambo ya ziwa katika nchi walimoishi Wagadarini.#8:28 Wagadarini Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagerasi” na zingine zina “Wagergesini”. Hapo wanaume wawili waliokuwa na mashetani ndani yao na kuishi makaburini walimwijia Yesu. Watu hao walikuwa hatari sana na watu hawakuitumia njia iliyopita karibu na makaburi yale. 29Wakapaza sauti na akasema, “Unataka nini kwetu, Mwana wa Mungu? Umekuja kutuadhibu kabla ya wakati uliopangwa?”
30Mbali kidogo na mahali hapo lilikuwepo kundi la nguruwe waliokuwa wanapata malisho yao. 31Mashetani yakamsihi Yesu yakasema, “Ikiwa utatufukuza kutoka ndani ya watu hawa, tafadhali tuache tuwaingie wale nguruwe.”
32Ndipo akawaamuru na akasema, “Nendeni!” Wale mashetani wakatoka ndani ya wale watu na kuwaingia nguruwe. Kisha kundi lote la nguruwe likaporomoka ziwani na nguruwe wote wakazama na kufa. 33Wachungaji waliokuwa wakiwachunga wale nguruwe wakakimbia. Wakaenda mjini na kuwaambia watu kila kitu kilichotukia, hasa juu ya wanaume wale wawili waliokuwa na mashetani. 34Kisha watu wote mjini walikwenda kumwona Yesu. Walipomwona, walimsihi aondoke katika eneo lao.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 8: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International