Luka 14
14
Je! ni Sahihi Kuponya Siku ya Sabato?
1Siku moja ya Sabato Yesu alikwenda nyumbani kwa miongoni mwa viongozi wa Mafarisayo kula chakula pamoja naye. Watu wote mahali pale walikuwa wanamwangalia kwa makini kuona atafanya nini. 2Mbele yake kulikuwa na mtu aliyekuwa na ugonjwa mbaya.#14:2 ugonjwa mbaya Yaani, “safura”, ugonjwa unaosababisha mwili kuvimba. 3Yesu akawauliza wanasheria na Mafarisayo, “Je! ni halali au kosa kuponya siku ya Sabato?” 4Lakini walishindwa kujibu swali lake. Hivyo akamshika yule mgonjwa, na kumponya, akamruhusu aende zake. 5Kisha akawaambia Mafarisayo na wanasheria, “Ikiwa mwanao au mnyama wako atatumbukia kisimani siku ya Sabato, mnatambua kuwa mtamtoa haraka.” 6Mafarisayo na wanasheria hawakuweza kujibu kinyume na alivyosema.
Usijifanye Mtu wa Muhimu
7Ndipo Yesu akagundua kuwa baadhi ya wageni walikuwa wanachagua sehemu za heshima za kukaa mezani. Ndipo akawaambia, 8“Ukialikwa na mtu katika sherehe ya harusi, usikae katika sehemu za heshima. Wanaweza kuwa wamemwalika mtu muhimu kuliko wewe. 9Na kama umekaa katika kiti muhimu zaidi, watakuja kwako na kukuambia ‘toka ulipokaa umpishe huyu!’ Ndipo itakulazimu kuhamia sehemu zisizo za heshima na utaaibika.
10Hivyo ukialikwa, nenda ukae mahali pasipo pa heshima, ili yule aliyekualika akija, akuambie, ‘Rafiki, njoo huku mbele zaidi mahali pazuri.’ Ndipo utaheshimiwa mbele ya wageni wote walio mezani pamoja nawe. 11Kila ajikwezaye atashushwa. Lakini ajishushaye atakwezwa.”
Utazawadiwa
12Kisha Yesu akamwambia Farisayo aliyemwalika, “Unapoandaa chakula, usiwaalike rafiki zako tu, au ndugu zako, au jamaa zako, wala jirani zako matajiri. Kwa sababu wao pia watakualika, na kwa kufanya hivyo watakuwa wanakulipa. 13Lakini ufanyapo sherehe waalike maskini, waliolemaa, walemavu wa miguu, na wasiyeona. 14Utabarikiwa, kwa sababu watu hawa hawana kitu cha kukulipa. Lakini Mungu atakupa thawabu wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
Mfano Kuhusu Watu Walioalikwa Kwenye Chakula
(Mt 22:1-10)
15Basi mmoja wa watu waliokuwa mezani pamoja naye aliposikia hayo akamwambia Yesu, “Wamebarikiwa watakaokula karamu katika ufalme wa Mungu.”
16Yesu akamwambia, “Mtu mmoja aliandaa sherehe kubwa, na kuwaalika watu wengi. 17Wakati wa kuanza sherehe ulipofika, alimtuma mtumishi wake awaambie wale walioalikwa, ‘Tafadhalini njooni sasa. Kila kitu kiko tayari.’ 18Lakini wageni waalikwa wote walisema kuwa hawawezi kuja. Kila mmoja alitoa udhuru. Wa kwanza alisema, ‘Nimenunua shamba, hivyo ni lazima niende nikalitazame. Tafadhali unisamehe.’ 19Mwingine alisema, ‘Nimenunua ng'ombe wa kulimia jozi tano; ni lazima niende kuwajaribu. Tafadhali unisamehe.’ 20Na mtu wa tatu alisema, ‘Nimeoa mke, kwa sababu hiyo siwezi kuja.’
21Hivyo mtumishi alirudi na kumjulisha bwana kilichotokea. Bwana wake akakasirika, akamwambia mtumishi wake, ‘Fanya haraka! Nenda mitaani na katika vichochoro vya mji. Niletee maskini, vilema, wasiyeona na walemavu wa miguu!’
22Baadaye mtumishi akamwambia, ‘Mkuu nimefanya kama ulivyoniagiza, lakini bado tuna nafasi kwa ajili ya watu wengine zaidi.’ 23Hivyo bwana wake akamwambia mtumishi, ‘Toka nje uende kwenye barabara zinazoelekea vijijini na kando ya mashamba. Waambie watu huko waje, ninataka nyumba yangu ijae! 24Ninakwambia, sitaki mtu hata mmoja kati ya wale niliowaalika kwanza atakayekula chakula hiki nilichoandaa.’”
Amua Ikiwa Unaweza Kunifuata
(Mt 10:37-38)
25Watu wengi walikuwa wanasafiri pamoja na Yesu. Akawaambia, 26“Ikiwa unakuja kwangu na hauko tayari kuiacha familia yako, huwezi kuwa mfuasi wangu. Ukimpenda zaidi baba yako, mama yako, mke wako, watoto wako, kaka na dada zako na hata maisha yako zaidi yangu huwezi kuwa mwanafunzi wangu. 27Yeyote ambaye hatauchukua msalaba atakaopewa na akanifuata, hawezi kuwa mfuasi wangu.
28Ikiwa unataka kujenga nyumba, kwanza utakaa na kuamua ili kujua itakugharimu kiasi gani. Ni lazima uone ikiwa una pesa za kutosha kumaliza kazi ya ujenzi. 29Usipofanya hivyo, unaweza ukaanza kazi, lakini ukashindwa kumaliza kujenga nyumba. Na usipoweza kuimaliza, kila mtu atakucheka, 30Watasema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, lakini alishindwa kumalizia.’
31Ikiwa mfalme anakwenda kupigana vita na mfalme mwingine, atakaa chini kwanza na kupanga. Ikiwa ana askari elfu kumi, ataamua ikiwa ana uwezo wa kumshinda mfalme mwenye askari elfu ishirini. 32Akiona hawezi kumshinda mfalme mwingine, atatuma baadhi ya watu kwa mfalme mwingine ili wapatane akiwa bado yuko mbali.
33Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wenu. Lazima uache kila kitu ulichonacho. La sivyo, huwezi kuwa mfuasi wangu.
Msipoteze Umuhimu Wenu
(Mt 5:13; Mk 9:50)
34Chumvi ni kitu kizuri; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, huwezi kuitengenezea ladha tena. 35Haifai. Huwezi hata kuitumia kama uchafu au mbolea. Watu huitupa tu.
Mnaonisikiliza, sikilizeni!”
Iliyochaguliwa sasa
Luka 14: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International