Luka 12
12
Msiwe Kama Mafarisayo
1Maelfu wengi wa watu walikusanyika. Walikuwepo watu wengi sana kiasi ambacho walikuwa wakikanyagana. Kabla Yesu hajaanza kuzungumza na watu wale, aliwaambia wafuasi wake, “Iweni waangalifu dhidi ya chachu ya Mafarisayo. Ninamaanisha kuwa hao ni wanafiki. 2Kila kitu kilichofichwa kitawekwa wazi, na kila kitu kilicho sirini kitajulikana. 3Mnachokisema sirini kitasemwa mbele za watu. Na mliyonong'onezana katika vyumba vyenu, yatahubiriwa sehemu za wazi ambako kila mtu atasikia.”
Mwogopeni Mungu, Siyo Watu
(Mt 10:28-31)
4Kisha Yesu akawaambia watu, “Ninawaambia ninyi, rafiki zangu, msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya chochote cha kuwaumiza. 5Mwogopeni Mungu maana Yeye ndiye mwenye nguvu ya kuwaua na kuwatupa Jehanamu. Ndiyo, mnapaswa kumwogopa yeye.
6Ndege wanapouzwa, ndege watano wadogo wanagharimu senti mbili tu za shaba. Lakini Mungu hasahau hata mmoja wao. 7Ndiyo, Mungu anajua hata idadi ya nywele mlizonazo kwenye vichwa vyenu. Msiogope ninyi ni wa thamani kuliko ndege wengi.
Msiionee Haya Imani Yenu
(Mt 10:32-33; 12:32; 10:19-20)
8Ninawaambia, mkinikiri mbele za watu, ndipo nami#12:8 nami Kwa maana ya kawaida, “Mwana wa Mtu” (Yesu Kristo). nitakiri kuwa ninyi ni wangu mbele za Mungu na malaika. 9Na atakayenikataa mimi mbele za watu, nami nitamkataa mbele za Mungu na malaika.
10Kila asemaye neno kinyume na Mwana wa Adamu atasamehewa. Lakini atakayesema kinyume na Roho Mtakatifu hatasamehewa.
11Watakapowapeleka ninyi katika masinagogi mbele ya viongozi na wenye mamlaka, msihangaike mtasema nini. 12Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”
Yesu Aaonya Kuhusu Ubinafsi
13Mmoja wa watu katika kundi akamwambia Yesu, “Mwalimu, baba yetu amefariki hivi karibuni na ametuachia vitu, mwambie kaka yangu anigawie baadhi ya vitu hivyo!”
14Lakini Yesu akamwambia, “Nani amesema mimi ni mwamuzi wa kuwaamulia namna ya ninyi wawili kugawana vitu vya baba yenu?” 15Ndipo Yesu akawaambia, “Iweni waangalifu na jilindeni dhidi ya kila aina ya ulafi. Maana uhai wa watu hautokani na vitu vingi wanavyomiliki.”
16Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Alikuwepo tajiri mmoja aliyekuwa na shamba. Shamba lake lilizaa mazao sana. 17Akasema moyoni mwake, ‘Nitafanya nini? Sina mahali pa kuyaweka mazao yangu yote?’
18Kisha akasema, ‘Ninajua nitakachofanya. Nitabomoa ghala zangu na kujenga ghala kubwa zaidi! Nitahifadhi nafaka zangu zote na vitu vingine vizuri katika ghala zangu mpya. 19Kisha nitajisemea mwenyewe, nina vitu vingi vizuri nilivyotunza kwa ajili ya kutumia kwa miaka mingi ijayo. Pumzika, kula, kunywa na furahia maisha!’
20Lakini Mungu akamwambia yule mtu, ‘Ewe mpumbavu! Leo usiku utakufa. Sasa vipi kuhusu vitu ulivyojiandalia? Nani atavichukua vitu hivyo?’
21Hivi ndivyo itakavyokuwa kwa mtu anayeweka vitu kwa ajili yake yeye peke yake. Mtu wa namna hiyo si tajiri kwa Mungu.”
Utangulizeni Kwanza Ufalme wa Mungu
(Mt 6:25-34,19-21)
22Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo ninawaambia, msisumbuke juu ya vitu mnavyohitaji kwa ajili ya kuishi, mtakula nini au mtavaa nini. 23Maisha ni muhimu zaidi ya chakula mnachokula na mwili ni zaidi ya mavazi mnayovaa. 24Waangalieni kunguru, hawapandi, hawavuni au kuweka katika majumba au ghala, lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani sana kuliko ndege. 25Hakuna mmoja wenu anayeweza kujiongezea muda katika maisha yake kwa kujihangaisha na maisha. 26Na ikiwa hamwezi kufanya mambo madogo, kwa nini mnajihangaisha kwa mambo makubwa?
27Yatafakarini maua yanavyoota. Hayafanyi kazi wala kujitengenezea mavazi. Lakini ninawaambia hata Sulemani, mfalme mkuu na tajiri, hakuvikwa vizuri kama maua haya. 28Ikiwa Mungu huyavika vizuri namna hii majani ya porini, mnadhani atawafanyia nini ninyi? Hilo ni jani tu, siku moja li hai na siku inayofuata linachomwa moto. Lakini Mungu huyajali kiasi cha kuyapendezesha. Hakika atafanya zaidi kwa ajili yenu. Imani yenu ni ndogo!
29Hivyo daima msijihangaishe na kile mtakachokula ama mtakachokunywa. Msisumbukie mambo haya. 30Hayo ndiyo mambo ambayo watu wote wasiomjua Mungu huyafikiria daima. Lakini Baba yenu anajua ya kuwa mnayahitaji mambo haya. 31Mnapaswa kufikiri kuhusu ufalme wa Mungu. Naye Mungu atawapa mambo mengine yote mnayohitaji.
Msitumainie Fedha
32Msiogope, enyi kundi dogo. Kwa kuwa imempendeza Baba yenu kuwapa ninyi ufalme wake. 33Uzeni vitu mlivyo navyo, wapeni fedha wale wanaohitaji. Hii ni njia pekee mnayoweza kufanya utajiri wenu usipotee. Mtakuwa mnaweka hazina isiyoisha mbinguni, mahali ambapo wezi hawawezi kuiba na hakuna wadudu wa kuharibu. 34Kwa kuwa mahali ilipo hazina yako, ndipo roho yako itakapokuwa.
Iweni Tayari Daima
(Mt 24:42-44)
35Iweni tayari! Vaeni kikamilifu na taa zenu zikiwaka. 36Iweni tayari kama watumishi wanaomngojea bwana wao anayerudi kutoka kwenye sherehe ya harusi. Bwana wao anaporudi na kubisha mlangoni, watumishi huweza kumfungulia mlango haraka. 37Bwana wao atakapoona kuwa wako tayari na wanamsubiri, itakuwa siku ya furaha kwa watumishi hao. Ninawaambia bila mashaka, bwana wao atavaa nguo, atawakaribisha kwenye chakula kisha atawahudumia. 38Watumishi hao wanaweza kumsubiri bwana wao mpaka usiku wa manane. Lakini watafurahi sana kwa sababu aliporudi aliwakuta bado wanamsubiri.
39Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua ni lini mwizi atakuja? Mnajua kuwa asingeruhusu mwizi akavunja na kuingia ndani. 40Hivyo, iweni tayari ninyi nanyi, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja wakati msiotarajia!”
Mtumwa Mwaminifu ni Yupi?
(Mt 24:45-51)
41Petro akasema, “Bwana, mfano ule ulikuwa kwa ajili yetu au kwa ajili ya watu wote?”
42Bwana akamjibu, “Fikiria kuhusu mtumishi mwenye hekima na mwaminifu, ambaye bwana wake anamwamini na kumweka kuwa msimamizi wa kuwapa watumishi wengine chakula kwa wakati uliokubalika? Mtumishi huyo ataoneshaje kuwa yeye ni msimamizi makini na anayeweza kujisimamia? 43Mkuu#12:43 Mkuu Yaani, “bwana wake”. Si Bwana ikimaanisha Yesu Kristo. wake atakaporudi na kumkuta akifanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha sana kwa mtumishi huyo. 44Ninawaambia ukweli bila mashaka yoyote, mkuu wake atamweka kuwa msimamizi wa vitu vyake vyote anavyomiliki.
45Lakini itakuwaje ikiwa mtumishi huyo ni mwovu na akadhani bwana wake hatarudi mapema? Ataanza kuwapiga watumishi wengine, wanaume na wanawake. Atakula na kunywa mpaka atalewa. 46Ndipo bwana wa mtumishi huyo atakuja wakati usiotarajiwa, wakati ambapo mtumishi hajajiandaa. Ataadhibiwa bila huruma#12:46 Ataadhibiwa bila huruma Kwa maana ya kawaida, “Kukatwa nusu”. na bwana wake na kumpeleka anakostahili, mahali waliko watumishi wengine wasiotii.
47Mtumishi huyo alijua kitu ambacho bwana wake alimtaka afanye. Lakini hakuwa tayari kufanya au kujaribu kufanya kile bwana wake alichotaka. Hivyo mtumishi huyo ataadhibiwa sana! 48Lakini vipi kuhusu mtumishi asiyejua kile ambacho bwana wake anataka? Yeye pia anafanya mambo yanayostahili adhabu, lakini ataadhibiwa kidogo kuliko mtumishi aliyejua alichotakiwa kufanya. Yeyote aliyepewa vingi atawajibika kwa vingi. Hivyo vingi vitategemewa kutoka kwa yule aliyepewa vingi zaidi.”
Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo
(Mt 10:34-36)
49Yesu aliendelea kusema: “Nimekuja kuleta moto ulimwenguni. Ninatamani ungekuwa unawaka tayari! 50Kuna aina ya ubatizo#12:50 ubatizo Neno hili ambalo maana yake ni kuzamishwa katika maji, limetumika hapa likiwa na maana maalumu ya tofauti, yaani kufunikwa au “kuzikwa” katika matatizo. ambao ni lazima niupitie na niteseke. Ninajisikia kusumbuka mpaka pale utakapotimizwa. 51Mnadhani nilikuja kuleta amani ulimwenguni? Hapana, nilikuja kuugawa ulimwengu! 52Kuanzia sasa, familia ya watu watano itagawanyika, watatu watakuwa kinyume cha wawili, na wawili kinyume cha watatu.
53Kina baba watakuwa kinyume cha wana wao:
na wana nao watakuwa kinyume cha baba zao.
Kina mama watakuwa kinyume cha binti zao:
na binti nao watakuwa kinyume cha mama zao.
Mama wakwe watakuwa kinyume cha wake za wana wao,
na wake za wana wao watakuwa kinyume cha mama wakwe zao.”#12:53 Tazama Mik 7:6.
Kuzielewa Nyakati
(Mt 16:2-3)
54Ndipo Yesu akawaambia watu, “Mnapoona wingu likikua upande wa magharibi, mnasema, ‘Mvua inakuja,’ na muda si mrefu huanza kunyesha. 55Mnapoona upepo unaanza kuvuma kutoka kusini mnasema, ‘Kutakuwa joto,’ na huwa hivyo. 56Enyi wanafiki! Mnaweza kuiona nchi na anga na mkajua hali ya hewa itakavyokuwa. Kwa nini hamwelewi kinachotokea sasa?
Malizeni Matatizo Yenu
(Mt 5:25-26)
57Kwa nini ninyi wenyewe hamwezi kujiamulia ninyi wenyewe kilicho haki? 58Ikiwa mtu anakushtaki na ninyi nyote mnaongozana kwenda mahakamani. Jitahidi kadri inavyowezekana kupatana naye mkiwa njiani. Usipopatana naye, atakupeleka kwa hakimu. Na hakimu atakutia hatiani na maofisa wa mahakama watakutupa gerezani. 59Ninawaambieni, hautatoka humo, mpaka ulipe kila senti unayodaiwa.”
Iliyochaguliwa sasa
Luka 12: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International