Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 2

2
Kuja kwa Roho Mtakatifu
1Siku ya Pentekoste ilipofika, wote walikuwa pamoja sehemu moja. 2Ghafla sauti ikaja kutoka mbinguni. Ilikuwa kama sauti ya upepo mkali unaovuma. Sauti hii ikajaa katika nyumba yote walimokuwa. 3Waliona miali iliyoonekana kama ndimi za moto. Miali ilitengana na kukaa juu ya kila mmoja wao pale. 4Wote walijaa Roho Mtakatifu na wakaanza kuzungumza kwa lugha tofauti. Roho Mtakatifu aliwapa uwezo wa kuzungumza lugha hizi.
5Wakati haya yanatokea, walikuwepo Wayahudi waliorudi makwao. Hawa walikuwa wacha Mungu kutoka kila taifa ulimwenguni waliokuja mjini Yerusalemu. 6Kundi kubwa lilikusanyika kwa sababu walisikia kelele. Walishangaa kwa sababu, mitume walipokuwa wakitamka maneno kila mtu alisikia kwa lugha ya kwao.
7Watu wote walilishangaa hili. Hawakuelewa ni kwa namna gani mitume waliweza kufanya hili. Wakaulizana, “Tazama! Watu wote hawa tunaowasikia wanatoka Galilaya.#2:7 wanatoka Galilaya Watu walidhani kuwa watu wanaotoka Galilaya walikuwa wanaweza kuzungumza lugha yao tu. 8Lakini tunawasikia wanatamka maneno kwa lugha zetu za asili. Hili linawezekanaje? Sisi tunatoka sehemu hizo mbalimbali: 9Parthia, Umedi, Elamu, Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto, Asia, 10Frigia, Pamfilia, Misri na maeneo ya Libya karibu na mji wa Kirene, Rumi, 11Krete na Uarabuni. Baadhi yetu ni Wayahudi kwa kuzaliwa na wengine si Wayahudi, bali wamechagua kumwabudu Mungu kama Wayahudi. Tunatoka katika nchi hizi mbalimbali, lakini tunawasikia watu hawa wakizungumza kwa lugha zetu tofauti! Sisi sote tunaweza kuelewa yote wanayosema kuhusu matendo makuu ya Mungu.”
12Watu wote walistaajabu na pia walichanganyikiwa. Wakaulizana, “Hii yote inamaanisha nini?” 13Lakini wengine waliwacheka mitume, wakisema wamelewa kwa mvinyo mwingi waliokunywa.
Petro Azungumza na Watu
14Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:
17‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
Vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18Katika siku hizo nitaimimina Roho
yangu kwa watumishi wangu,
wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19Nitafanya maajabu juu angani.
Nitasababisha ishara chini duniani.
Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20Jua litakuwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21Na kila amwombaye Bwana’#2:21 kila amwombaye Bwana Kwa maana ya kawaida, “kila aliitiaye jina la Bwana”. ataokolewa.#Yoe 2:28-32
22Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia. 25Daudi alilisema hili kuhusu Yesu:
‘Sijasahau kuwa Bwana yu pamoja nami.
Yupo hapa pembeni yangu,
hivyo hakuna kinachoweza kunidhuru.
26Ndiyo sababu ninafurahi sana,
na ninaimba kwa furaha!
Lipo tumaini hata kwa ajili ya mwili wangu huu dhaifu,
27kwa sababu wewe Bwana hutaniacha kaburini.#2:27 kaburini Kwa maana ya kawaida, “Kuzimu”. Pia katika mstari wa 31.
Hautauacha mwili wa mtumishi wako mwaminifu#2:27 mtumishi wako mwaminifu Au “Mtakatifu wako”, kwa kawaida neno hili linamaanisha mtu aliyejitoa na kumpendeza Mungu. kuozea huko.
28Umenionyesha njia iendayo uzimani.
Kuwa pamoja nawe kutanijaza furaha.’#Zab 16:8-11
29Ndugu zangu, ninaweza kuwaambia kwa ujasiri kuhusu Daudi, baba yetu mkuu. Alikufa, akazikwa, na kaburi lake liko hapa pamoja nasi hata leo. 30Alikuwa nabii na alijua kitu ambacho Mungu alisema. Mungu alimwahidi Daudi kwa kuweka Agano kuwa mzaliwa katika familia yake mwenyewe ataketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi kama mfalme.#2:30 Mungu alimwahidi … kama mfalme Tazama 2 Sam 7:12,13 na Zab 132:11. 31Daudi aliliona hili kabla halijatokea. Ndiyo maana alisema hivi kuhusu mfalme anayekuja:
‘Hakuachwa kaburini.
Mwili wake haukuozea humo.’#2:31 Tazama Zab 16:10.
Daudi alizungumza kuhusu Masihi kufufuka kutoka kwa wafu. 32Yesu ndiye ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi sote ni mashahidi wa jambo hili. Tulimwona. 33Yesu alichukuliwa juu mbinguni. Na sasa ameketi upande wa kulia wa Mungu. Baba amempa Roho Mtakatifu, kama alivyoahidi. Hivyo Yesu amemimina huyo Roho Mtakatifu na hiki ndicho mnachoona na kusikia 34Daudi hakuchukuliwa mpaka mbinguni. Daudi mwenyewe alisema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kuume
35hadi nitakapowaweka maadui zako chini ya udhibiti wako.’#2:35 hadi nitakapowaweka … udhibiti wako Kwa maana ya kawaida, “mpaka nitakapowafanya adui zako kuwa sehemu ya kuweka miguu yako”. #Zab 110:1
36Hivyo, watu wote wa Israeli wanapaswa kulijua hili bila kuwa na mashaka: Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Masihi. Ndiye yule mliyempigilia msalabani!”
37Watu waliposikia hili wakahuzunika sana. Wakawauliza Petro na mitume wengine, “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38Petro akawaambia, “Geuzeni mioyo na maisha yenu na kila mmoja wenu abatizwe katika jina la Yesu Kristo. Ndipo Mungu atawasamehe dhambi zenu, na mtapokea zawadi ya Roho Mtakatifu. 39Ahadi hii ni kwa ajili yenu ninyi, watoto wenu na vizazi vijavyo. Ni kwa kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake mwenyewe.”
40Petro aliwaonya kwa maneno mengine mengi; aliwasihi, akawaambia, “Jiokoeni na uovu unaofanywa na watu wanaoishi sasa!” 41Ndipo wale walioyakubali yale aliyosema Petro wakabatizwa. Yapata watu elfu tatu waliongezwa kwenye kundi la waamini siku ile.
Ushirika wa Waamini
42Waamini walitumia muda wao kusikiliza mafundisho ya mitume. Walishirikiana kila kitu kwa pamoja. Walikula#2:42 Walikula Kwa maana ya kawaida, “Walimega mkate”. Hii inaweza kumaanisha mlo, chakula cha kawaida au Meza ya Bwana, mlo maalumu ambao Yesu aliwaambia wafuasi wake wale kwa ajili ya kumkumbuka yeye. Pia katika mstari wa 46. Tazama Lk 22:14-20. na kuomba pamoja. 43Maajabu mengi na ishara nyingi zilikuwa zinatokea kupitia mitume, na hivyo kila mtu aliingiwa na hofu na akamtukuza Mungu. 44Waamini wote walikaa pamoja, na kushirikiana kila kitu. 45Waliuza mashamba yao na vitu walivyomiliki, kisha wakatoa fedha na kuwapa wenye kuhitaji. 46Waamini waliendelea kukutana pamoja katika eneo la Hekalu. Pia walikula pamoja katika nyumba zao. Walikuwa na furaha kushirikiana chakula chao na walikula kwa mioyo mikunjufu. 47Waamini walimsifu Mungu na waliheshimiwa na watu wote. Watu wengi zaidi waliokolewa kila siku, na Bwana alikuwa akiwaongeza kwenye kundi lao.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 2: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia