Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yakobo 4

4
Urafiki na ulimwengu
1Mapigano na ugomvi wote kati yenu vinatoka wapi? Hutoka katika tamaa zenu mbaya ambazo hupigana daima ndani yenu. 2Mnatamani vitu na kwa vile hamvipati mko tayari kuua; mwatamani sana kupata vitu, lakini hamvipati; hivyo mnagombana na kupigana. Hampati kile mnachotaka kwa sababu hamkiombi kwa Mungu. 3Tena, mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya; mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu. 4Nyinyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi.#4:4 Watu …kama wazinzi: Katika vitabu vya manabii wa A.K. ukosefu wa uaminifu katika ndoa ulikuwa mfano wa ukosefu wa uaminifu kwa Mungu kwa upande wa taifa lake la Israeli ambalo lilichukuliwa kama mchumba wake Mwenyezi-Mungu (Isa 1:21; Yer 3:6—10:20; Eze 16; Hos 2:2). Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu#4:4 Rafiki wa ulimwengu: Taz Yoh 1:10 maelezo; rejea Rom 8:7; 1Yoh 2:15-16. Hapa pia neno “ulimwengu” linatumiwa kutaja watu au nguvu zinazopingana na Mungu na watu wake. ni kuwa adui wa Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu. 5Msifikiri kwamba Maandiko Matakatifu yamesema maneno ya bure, yanaposema: “Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu ana wivu mkubwa.”#4:5 Moja ya aya ngumu katika barua hii ya Yakobo. Mwandishi ananukuu kutoka makala ambayo hatuijui. Tafsiri iliyotolewa hapa ni yamkini. Roho, yaani Roho Mtakatifu, anakuwa na wivu kama mume (au mke) anapokuwa na wivu amwonapo mkewe (au mumewe) anawaandama watu wengine kama ilivyotajwa katika aya iliyotangulia. Wengine wanaelewa roho hapa kuwa ni roho ya binadamu na wanatoa tafsiri tofauti k.m. “Roho ambayo Mungu aliiweka ndani yetu ina hamu ya miungu”. 6Lakini, neema tunayopewa na Mungu ina nguvu zaidi; kama yasemavyo Maandiko: “Mungu huwapinga wenye majivuno lakini huwapa neema wanyenyekevu.”#4:6 Mungu huwapinga wenye majivuno …huwapa neema wanyenyekevu: Meth 3:34 (Kigiriki); imenukuliwa pia katika 1Pet 5:5 (rejea Yak 4:10; Mat 23:12).
7Basi, jiwekeni chini ya Mungu; mpingeni Ibilisi naye atawakimbieni. 8Mkaribieni Mungu, naye atakuja karibu nanyi. Osheni mikono yenu enyi wakosefu! Safisheni mioyo yenu enyi wanafiki!#4:8 Enyi wanafiki: Au, “Wenye nia mbili”; taz Yak 1:8. 9Oneni huzuni, lieni na kuomboleza; kicheko chenu na kiwe kilio; na furaha yenu iwe huzuni kubwa. 10Nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni.
Onyo kuhusu kumhukumu ndugu
11Ndugu, msilaumiane nyinyi kwa nyinyi. Anayemlaumu ndugu yake na kumhukumu, huyo huilaumu na kuihukumu sheria. Kama ukiihukumu sheria, basi, wewe huitii sheria, bali waihukumu. 12Mungu peke yake ndiye mwenye kuweka sheria na kuhukumu. Ni yeye peke yake anayeweza kuokoa na kuangamiza. Basi, wewe ni nani hata umhukumu binadamu mwenzako?
Onyo kuhusu majivuno
13Basi, sasa sikilizeni nyinyi mnaosema: “Leo au kesho tutakwenda katika mji fulani na kukaa huko mwaka mzima tukifanya biashara na kupata faida.” 14Nyinyi hamjui hata maisha yenu yatakavyokuwa kesho!#4:13-14 Hamjui …maisha yenu … kesho: Tafsiri nyingine yamkini: “Hamjui yatakayotokea kesho wala maisha yenu yatakuwaje”. (Rejea Meth 27:1). Nyinyi ni kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi tu na kutoweka tena. 15Mngalipaswa kusema: “Bwana akitujalia tutaishi na tutafanya hiki au kile.” 16Lakini sasa mwajivuna na kujigamba; majivuno ya namna hiyo ni mabaya.
17Basi, mtu ambaye hafanyi lile jambo jema analojua kwamba anapaswa kulifanya, anatenda dhambi.

Iliyochaguliwa sasa

Yakobo 4: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia