Yakobo 2
2
Onyo kuhusu ubaguzi
1Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu,#2:1 Bwana wa utukufu: Au, “Bwana Mtukufu”. Taz 1Kor 2:8 maelezo. msiwabague watu kamwe.#2:2-3 Matajiri hao wanaotajwa katika 2:2—3:6; 5:1 labda ni watu wasio waumini (ling 2:7). 2Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.#2:2-3 Kwa kutumia maneno mazitomazito, aya hizi zinalaumu na kupatiliza ubaguzi wowote ule kwa vile matendo ya namna hiyo yanapingana dhahiri na sheria na matakwa ya Injili. Taz Yak 1:9-10 maelezo. 3Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,” 4je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu#2:5 Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu: Rejea Luka 6:20 na pia Isa 66:2. huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea ufalme aliowaahidia wale wanaompenda. 6Lakini nyinyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamiza na kuwapeleka mahakamani? 7Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri#2:7 Wanaolitukana hilo jina lenu zuri: Hilo jina ni jina la Yesu Kristo, ambalo lilitamkwa juu ya waumini wakati wa ubatizo (rejea Mate 2:38; 10:48). Matajiri ambao walisema vibaya juu ya jina hilo walikuwa watu wasio Wakristo. mlilopewa?
8Kama mnaitimiza ile sheria ya ufalme kama ilivyoandikwa katika Maandiko Matakatifu: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”, mtakuwa mnafanya vema kabisa.#2:8 Lawi 19:18. Rejea nukuu hiyohiyo iliyofanywa na Yesu (Mat 22:39-40) vilevile na Paulo (Rom 13:9-10). 9Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo sheria inawahukumu nyinyi kuwa mna hatia. 10Anayevunja amri mojawapo ya sheria, atakuwa na hatia ya kuivunja sheria yote. 11Maana yuleyule aliyesema: “Usizini,” alisema pia “Usiue.”#2:11 “Usizini… Usiue”: Kut 20:13-14; Kumb 5:17-18; ling Mat 5:21-22. Kwa hiyo, hata ikiwa hukuzini, lakini umeua, wewe umeivunja sheria. 12Basi, semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria iletayo uhuru.#2:12 Sheria iletayo uhuru: Taz Yak 1:25 maelezo. 13Maana, Mungu hatakuwa na huruma atakapomhukumu mtu asiyekuwa na huruma.#2:13 Hatakuwa na huruma …mtu asiyekuwa na huruma: Rejea Mat 6:14-15; 18:23-35. Lakini huruma hushinda hukumu.#2:13 Huruma hushinda hukumu: Rejea Mat 5:7; 7:2.
Imani na matendo
14Ndugu zangu, kuna faida gani mtu kusema ana imani, lakini haonyeshi kwa vitendo? Je, hiyo imani yawezaje kumwokoa?#2:14 Hapa yahusu imani ya nje nje tu, au kuhusu kukubali kwa akili tu kweli za kidini bila kumtii Mungu kwa vitendo. Yakobo anabainisha mtu mwenye imani hiyo tupu (ya kiakili) na mtu mwenye imani hai ambayo yaonekana kwa matendo. Rejea Mat 7:21; Gal 5:6; Yak 1:22 na taz pia Yak 1:3 maelezo. 15Tuseme kaka au dada hana nguo au chakula. 16Yafaa kitu gani nyinyi kuwaambia hao: “Nendeni salama mkaote moto na kushiba,” bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? 17Vivyo hivyo, imani peke yake bila matendo imekufa.
18Lakini mtu anaweza kusema: “Wewe unayo imani, mimi ninayo matendo!” Haya! Nioneshe jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani bila matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo yangu. 19Je, wewe unaamini kwamba yuko Mungu mmoja? Sawa! Lakini hata pepo huamini hilo, na hutetemeka kwa hofu. 20Mpumbavu wee! Je, wataka kuoneshwa kwamba imani bila matendo imekufa? 21Je, Abrahamu babu yetu alipataje kukubaliwa kuwa mwadilifu? Kwa matendo yake, wakati alipomtoa tambiko mwanawe Isaka juu ya madhabahu. 22Waona, basi, kwamba imani yake iliandamana na matendo yake; imani yake ilikamilishwa kwa matendo yake. 23Hivyo yakatimia yale Maandiko Matakatifu yasemayo: “Abrahamu alimwamini Mungu, na kwa imani yake akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu;#2:23 Abrahamu alimwamini Mungu …akakubaliwa kuwa mtu mwadilifu: Mwa 15:6; taz pia Ebr 11:8-11,17-19. na hivyo Abrahamu akaitwa rafiki ya Mungu.”#2:23 Rafiki ya Mungu: Rejea 2Nya k 20:7; Isa 41:8. 24Mnaona, basi, kwamba mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa matendo yake, na si kwa imani peke yake.
25Ilikuwa vivyo hivyo kuhusu yule malaya Rahabu; yeye alikubaliwa kuwa mwadilifu kwa sababu aliwapokea wale wapelelezi na kuwasaidia waende zao kwa kupitia njia nyingine.#2:25 Yos 2:1-21; 6:17; taz Ebr 11:31 ambapo kitendo cha Rahabu kinatajwa kama kitendo sawa kilichofanywa kwa imani.
26Basi, kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa.
Iliyochaguliwa sasa
Yakobo 2: BHNTLK
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993