Mwanzo 2
2
1Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyokamilika pamoja na vitu vyote vilivyomo. 2Siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyofanya; siku hiyo ya saba Mungu akapumzika#2:2 Mungu akapumzika: Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa kwa kitenzi “akapumzika” lina maana: “akaacha” au “akamaliza”. Kwa kusema kwamba Mungu alipumzika haina maana ya kwamba yeye aliacha kutenda ila ina maana kwamba yote aliyotenda yalifana kulingana na yale aliyokusudia. Taz Yoh 5:17-18 maelezo. baada ya kazi yake yote aliyofanya. 3Mungu akaibariki siku ya saba#2:3 Siku ya saba: Katika Biblia namba au idadi saba inatumika mara nyingi kuelezea ukamilifu wa kitu. Taz Mwa 4:18 maelezo. na kuitakasa, kwa kuwa siku hiyo Mungu alipumzika baada ya kazi yake yote ya kuumba. 4Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa.#2:4 Hivyo ndivyo mbingu na dunia zilivyoumbwa: Hapa wazo la Mwa 1:1 linarudiwa ili kuonesha kwamba simulizi la kuumbwa ulimwengu limekamilika. Tafsiri au fafanuzi mbalimbali zimetolewa kuhusu tamko hili. Katika Kiebrania, neno kwa neno, ni: Hivi ni vizazi vya mbingu na dunia zilipoumbwa. Lakini “vizazi” hapa, yamkini ni msemo unaokusudia kutaja vitu vyote vya ulimwengu. Kwa hiyo si vizazi vya binadamu. Tafsiri nyingine zimejaribu kuleta maana kwa kusema: “Hii ndiyo historia ya mbingu na dunia zilipoumbwa”. Tafsiri nyingine pia hufikiri kwamba mwandishi alitaka kusema “jinsi zilivyoumbwa”, lakini mwandishi hana nia ya kusema juu ya “namna”, bali anasema tu wakati “zilipoumbwa” hivyo ndivyo vitu vyake vya awali, vizazi vyake au historia yake. Mtendaji wa “zilipoumbwa” bila shaka ni Mungu, na tafsiri nyingine ni “wakati Mungu alipoziumba”. Kwa namna hii tamko hili linaifunga sehemu iliyotangulia kwa kurudia tena ile mada ya 1:1.
Bustani ya Edeni#2:4b-25 Simulizi linalofuata (2:4-25), tofauti na 1:1—2:4a, linahusu kwa namna ya pekee kuumbwa kwa mwanamume na mwanamke.
Siku ile Mwenyezi-Mungu#2:4 Mwenyezi-Mungu: Kwa mara ya kwanza jina la Mungu (Kiebrania, “Yahweh”) linatumiwa. Jina lingine la Mungu, hasa katika manabii ni “Mwenyezi-Mungu wa Majeshi”. Tafsiri nyingine za Kiswahili zinatumia neno “Bwana” kila mara jina “Yahweh” linapotumiwa katika A.K. Shida kubwa katika Kiswahili ni kwamba neno “Bwana”, hata kama likiandikwa kwa herufi kubwa zote, ni neno kisifa la kumtaja mwanamume mzima kutofautisha na mwanamke mzima: Bwana fulani, Bibi fulani. Kwa sababu hiyo, ili kuleta maana ile ya awali ya kumtaja Mungu, tafsiri hii imetumia jina kamili la Kiswahili la kumtaja huyo Mungu wa pekee, Muumba, na ambaye hakuna mwingine. Jina lenyewe ni Mwenyezi-Mungu. Tafsiri ya Kigiriki ijulikanayo kama Septuajinta (LXX) inatumia neno “Kurios” pale ambapo “Yahweh” linatumiwa katika Kiebrania na pia pale ambapo neno lingine la Kiebrania “adon” (adonay) linalotumiwa. Neno hilo la Kiebrania “adon” Kiswahili ni “Bwana”. Kwa hiyo pale katika A.K. (na pia A.J.) ambapo neno hilo linatumika kumtaja Mungu (na pia katika A.J. kumtaja Yesu Kristo) tafsiri hii inatumia neno “Bwana”. Kwa maelezo zaidi, Taz Mwa 4:26 maelezo, na Kut 3:14-15 na maelezo yake. alipoziumba mbingu na dunia, 5Hapakuwa na mimea juu ya nchi wala miti haikuwa imechipua kwani Mwenyezi-Mungu hakuwa ameinyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima. 6Hata hivyo, maji yalitoka ardhini yakainywesha ardhi yote. 7Basi, Mwenyezi-Mungu akamfanya mwanamume kwa mavumbi ya udongo,#2:7 Akamwumba mtu kwa udongo: Kiebrania kinatumia mchezo wa maneno hapa: “adam” neno ambalo lina maana ya “mtu” (binadamu) na “adama” neno ambalo lina maana ya “udongo.” (Mtindo huohuo unatumiwa katika Mwa 3:19). Yahusu uhusiano uliopo kati ya binadamu na nchi au udongo. akampulizia puani pumzi ya uhai,#2:7 Akampulizia …pumzi ya uhai: Kutaja kitendo hiki cha pekee cha Mungu kunakumbusha tofauti iliyopo baina ya kuumbwa viumbe vingine na binadamu (taz lugha inayotumiwa katika Mwa 1:27). Rejea Isa 45:9-11; Yer 18:1-6; Rom 9:21 ambapo kitendo kikuu cha Mungu kinafananishwa na mfinyanzi anayefinyanga vyombo vyake. na huyo mwanamume akawa kiumbe hai.
8Kisha Mwenyezi-Mungu akapanda bustani huko Edeni,#2:8 Edeni: Jina hili Kiebrania maana yake ni “enye kupendeza sana” au, “anasa” (rejea Isa 51:3; Eze 31:8-9). Wengine wanahusisha jina hilo na neno la lugha ya Asiria lenye maana ya tambarare, nyika au mbuga. upande wa mashariki, na humo akamweka huyo mwanamume aliyemuumba. 9Mwenyezi-Mungu akaotesha kutoka ardhini kila aina ya miti mizuri izaayo matunda yafaayo kwa chakula. Katikati ya bustani hiyo kulikuwa na mti wa uhai#2:9 Mti wa uhai: Au, “Mti ambao matunda yake huleta uhai”. Rejea Mwa 3:22; Ufu 2:7; 22:2,14. na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.#2:9 Mti wa ujuzi wa mema na mabaya: Ili kuweza kuelewa vizuri maana ya maneno haya yafaa kukumbusha tena desturi katika lugha ya Kiebrania ya kutaja jumla ya kitu au ukamilifu wa kitu kwa kutaja maneno mawili yanayoonesha pande mbili za hicho kitu ambazo zinakabiliana (taz k.m. maelezo ya 1:1). Fungu hili la maneno halina maana ya ujuzi wa akili peke yake, ila laweza pia kujumlisha wazo la utambuzi, upambanuzi na hata pia wazo la kumiliki. Kujua mema na mabaya aghalabu ni sawa na kuweza kuamua kwa hiari na bila kumtegemea mwingine kilicho chema au kilicho kibaya; kwa maneno mengine ni sawa na kuwa na mamlaka kamili kuhusu jambo la uadilifu. Rejea Mwa 3:22.
10Kulikuwa na mto huko Edeni uliotiririka maji na kuinywesha hiyo bustani; kutoka huko mto huo uligawanyika kuwa mito minne. 11Jina la mto wa kwanza ni Pishoni; huo waizunguka nchi yote ya Hawila ambako kuna dhahabu. 12Dhahabu ya nchi hiyo ni safi kabisa. Huko pia kuna marashi yaitwayo bedola na vito viitwavyo shohamu. 13Jina la mto wa pili ni Gihoni; huo waizunguka nchi yote ya Kushi.#2:10-14 Si wazi, dhahiri ni mahali gani hasa panapohusika katika simulizi hili. Kushi ni eneo la Afrika ya kaskazini (ambapo sasa ni Misri, Ethiopia mpaka hata Sudani) na mto Gihoni unadhaniwa kuwa ni Nili, hali Tigri na Eufrate ni mito ya huko Mesopotamia. 14Jina la mto wa tatu ni Tigri, nao watiririkia upande wa mashariki wa nchi ya Ashuru; na jina la mto wa nne ni Eufrate.
15Basi, Mwenyezi-Mungu akamtwaa huyo mwanamume, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.#2:15 Ailime na kuitunza: Hapa, kazi sio matokeo ya adhabu kwa dhambi ila ni shughuli inayomwezesha mtu kutekeleza wajibu katika kuhifadhi maendeleo ya dunia na pia kujiendeleza yeye mwenyewe (rejea Mwa 1:28). Ni kutokana tu na dhambi ndipo jambo la kazi limechukua hali yake ya bughudha, jasho na taabu (Mwa 3:17,19). 16Mwenyezi-Mungu alimwamuru huyo mwanamume, “Waweza kula matunda ya mti wowote katika bustani; 17lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, usile,#2:17 Matunda ya mti wa ujuzi …usile: Kwa kumpa amri hiyo Mungu anatambua kwamba huyo mtu ni kiumbe anayewajibika kwa vitendo vyake; na kwa upande mwingine pia Mungu anaonesha ukuu wake juu ya binadamu na kumtaka atambue mpaka wake yeye mwenyewe na mazingira yake ya kibinadamu (Eze 28:2; rejea Isa 14:13-14). maana siku utakapokula matunda ya mti huo, hakika utakufa.”
18Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Si vizuri huyu mwanamume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa#2:18 Msaidizi: Tafsiri nyingine yamkini ni “mwenzi”. kumfaa.” 19Basi, kutoka katika udongo, Mwenyezi-Mungu akaumba kila mnyama wa porini na kila ndege wa angani, halafu akamletea huyo mwanamume aone atawapa majina gani; na majina aliyowapa viumbe hao, yakawa ndio majina yao.#2:19-20 Majina aliyowapa …yakawa ndio majina yao: Jina la kitu, kwa fikira za watu wa Mashariki ya Kati ya Kale, halikuwa tu jambo la nje nje tu, ila lilikuwa sehemu ya maumbile ya mtu au kitu hicho kinachopewa jina hilo. Kuitia jina au kubadili jina ilimaanisha pengine kuwa na mamlaka kiasi fulani juu ya huyo mtu au kitu (taz k.m. 2Fal 23:34). 20Basi, huyo mwanamume akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, wanyama wa porini na ndege wote wa angani. Lakini hakupatikana msaidizi yeyote wa kumfaa.
21Basi, Mwenyezi-Mungu akamletea huyo mwanamume usingizi mzito, na alipokuwa usingizini, akatwaa ubavu wake mmoja na kupafunika mahali pale kwa nyama. 22Na huo ubavu Mwenyezi-Mungu alioutoa kwa yule mwanamume akaufanya kuwa mwanamke, akamleta kwa huyo mwanamume. 23Ndipo huyo mwanamume akasema,
“Naam! Huyu ni mfupa kutoka mifupa yangu,
na nyama kutoka nyama yangu.
Huyu ataitwa ‘Mwanamke’,#2:23 Aya hii ina madhumuni dhahiri ya kuonesha kwamba huyo mwanamke na huyo mwanamume chimbuko lao ni moja. Maneno “mwanamume” … “mwanamke” katika Kiebrania matamshi yake yanafanana: “ish” na “ishah”.
kwa sababu ametolewa katika mwanamume.”
24Ndiyo maana mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe,#2:24 Mwanamume humwacha baba yake na mama yake, akaambatana na mkewe: Mat 19:5; Marko 10:7-8; 1Kor 6:16; Efe 5:31. Aya hii inatilia mkazo ubora na maana ya ndani kabisa ya ndoa. nao wawili huwa mwili mmoja.
25Huyo mwanamume na mkewe wote walikuwa uchi, lakini hawakuona haya.#2:25 Walikuwa uchi, lakini hawakuona haya: Kuwa uchi hapa bila kuona haya ni maelezo ya hali timilifu isiyo na kasoro au hisia ya hatia; hali ya amani wao kwa wao, na wao wenyewe na Mungu. Baadaye lakini, kama matokeo ya dhambi, inakuwa hali ya haya na aibu.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 2: BHNTLK
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993