Wimbo ulio Bora UTANGULIZI
UTANGULIZI
Katika Kiebrania kitabu hiki huitwa “Wimbo Mkuu”, “Wimbo wa Nyimbo” au “Wimbo bora”. Maana yake ikiwa wimbo ulio mzuri kupita zote.
Wimbo Ulio Bora ni mkusanyo wa tenzi ambazo kwa ujumla wake zinahusu mahaba kati ya mume na mke. Katika historia ya mafafanuzi yake kumekuweko maelezo matatu makuu: Kwanza ni maelezo juu ya Sulemani na msichana Mshulami (6:3) waliopendana wakaoana. Pili, ni juu ya kijana mfugaji, rafiki yake Mshulami ambaye walipendana sana; lakini mfalme alimnyang'anya kijana mfugaji muhibu wake halafu mfalme akajitahidi kuvuta mapenzi yake huyo Mshulami hata ingawa hakufaulu. Tatu ni hadithi inayoeleza kwa njia ya kiistiari upendo wa Mungu kwa taifa lake (Hos. 2). Wazo hili liliegemea mapokeo ya kitabu hiki kusomwa rasmi kwenye ibada za sikukuu ya Pasaka katika masinagogi ya Wayahudi. Mwanzoni mwa Agano Jipya maelezo hayo yalipanuliwa yakawa upendo wa Kristo na kanisa lake.
Mwandishi wake afikiriwa kuwa mfalme Sulemani (1 Fal 4:29-34) maana kuna madokezo kadhaa kuhusu fikira hii (1:1,5; 3:7-11; 8:11-12; 1 Fal 11:1-41). Hata hivyo, utenzi wote haumhusu Sulemani. Nyimbo kadhaa zatokana na mtu mmoja na nyingine watu mbalimbali. Nazo zilikusanywa baada ya Wayahudi kutoka uhamishoni Babeli.
Kitabu hiki chasifia mapenzi ya kweli kati ya mwanamume na mwanamke. Suala hili laonekana kuwa si la kibinadamu peke yake ni la kimungu pia. Mungu amebariki upendo wa ndoa. Uhusiano kati ya mume na mke ni halali na bora. Mwingine yeyote yule haruhusiwi kuingilia ndoa (2:16; 7:10).
Yaliyomo:
1. Hamu ya kumwona rafiki na sifa zao, Sura 1:1—2:7
2. Nyimbo tatu za kumbukumbu na ndoto, Sura 2:8—6:3
3. Wimbo wa hamu ya kuwa pamoja, Sura 6:4—8:4
4. Nguvu ya upendo wa kweli na thawabu yake, Sura 8:5-14
Iliyochaguliwa sasa
Wimbo ulio Bora UTANGULIZI: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.