Ruthu 1:1-21
Ruthu 1:1-21 SRUV
Hapo zamani Waamuzi walipokuwa wanatawala, njaa ilitokea katika nchi. Mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaondoka akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrata wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. Nao wakaoa wanawake wa Kimoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthu. Baada ya kukakaa huko miaka kumi hivi, wote wawili Maloni na Kilioni wakafa; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana akiwa katika nchi ya Moabu alipata habari kuwa BWANA alikuwa amewajia watu wake na kuwapa chakula. Basi akatoka pale alipokuwa akiishi, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, rudini; kwa nini mfuatane nami? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu. Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye. Naye akasema, Tazama, dada yako amerudi kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urudi nawe ukamfuate dada yako. Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirudi nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; Pale utakapofia ndipo nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; BWANA anitende vivyo hivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. Basi alipomwona kuwa amekata shauri kufuatana naye, aliacha kumshawishi. Hivyo hao wakaendelea wote wawili hadi walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote uliwaajabia. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi? Akawaambia, Msiniite Naomi, niiteni Mara kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. Mimi nilitoka nikiwa nimejaa, naye BWANA amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa BWANA ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?