Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 3:1-20

Warumi 3:1-20 SRUV

Basi Myahudi ana nini zaidi? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutoamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? La hasha! Mungu aonekane kuwa kweli japo kila mtu ni mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulikane kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.) Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi? Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki. Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wagiriki ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira iko chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.

Soma Warumi 3

Video ya Warumi 3:1-20

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Warumi 3:1-20